Header Ads Widget

MISAFARA, MIKOPO YA SAMIA YAMKERA SUGU, HAONGA ALIA NA UTITIRI WA TOZO KWENYE KILIMO.

 


NA JOSEA SINKALA, SONGWE.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi (Sugu), ameeleza kukerwa na kitendo cha Serikali ya Tanzania kuendelea kukopa mikopo na kutumika vibaya badala ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.


Mwenyekiti huyo wa CHADEMA upande wa Kanda ya Nyasa ametoa kilio chake hicho wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Isansa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.


Sugu amesema Taifa limekuwa na viongozi wanaopenda anasa kwa kununua magari ya kifahari kwa ajili ya watumishi wakuu hasa mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi huku hali ikiendelea kuwa ngumu kwa mwananchi wa kawaida.


Amekosoa safari za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anazokwenda nje ya nchi akiwa na msururu wa watu jambo analosema ni ufujaji fedha za wa-Tanzania.


Pamoja na hayo amewatuhumu baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri kufuja fedha za umma ikiwemo zinazokopwa nje ya nchi.


"Wanakopa fedha nje ya nchi, zinakuja Tanzania halafu wanazipiga, wanajenga nyumba za kifahari, wananunua majumba Dubai, wananunua majumba Capetown Afrika kusini lakini inapofika kulipa lile deni la Taifa ni mimi na wewe na yule na dadaangu hapo na mtoto huyu anakua deni analikuta atalipa. Deni la Taifa linaongezeka wakati wanaonufaika ni wachache sidhani kama wanafika hata elfu moja wanaonufaika na nchi hii. Ndio maana CCM haitaki Katiba mpya kwasababu inawasaidia kuendelea kubaki madarakani", amesema Joseph Mbilinyi, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa.


Pamoja na hayo kiongozi huyo wa upinzani amewataka wananchi kuendelea kujiandaa na chaguzi zijazo ili kufanya mabadiliko kwa kuchagua viongozi bora kwenye Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji pamoja na uchaguzi mkuu mwakani ikiwemo kuhakikisha majimbo yasiyopungua ishirini kati ya thelathini na moja ya Kanda yake yanakwenda CHADEMA.


"Ni kweli tulimwambia Magufuli (Rais awamu ya tano) kula ndege toka nje uone kinachofanyika Duniani lakini hatukumaanisha haya wanayoyafanya, haitakiwi Rais anaenda ziara (nje) anaenda na watu hamsini watu sitini watu wamejaa kwenye ndege mpaka machawa wanaenda kufanya nini matokeo yake wanapata aibu tu zinarudi picha Rais wetu (Dkt.Samia Suluhu) amekaa na watu kama themanini halafu watu walioenda kuwaomba hela wamekaa kama sita tu!", ameeleza Sugu.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya CHADEMA Digital Kanda ya Nyasa ambaye alikuwa mgombea ubunge wa jimbo la Mbozi Pascal Yohana Haonga, amesema ni lazima wananchi wafanye mabadiliko kwenye chaguzi zijazo akisema hali ya wananchi imezidi kuwa mbaya.


Mbunge huyo wa zamani wa Mbozi amesema uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 uliporwa hivyo wananchi kukosa wawakilishi sahihi na ndio maana wanaendelea kughubikwa na kero mbalimbali ikiwemo utitiri wa kodi, tozo na ushuru hata kwenye mazao sanjari na ubovu wa barabara ambazo ziliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini mpaka sasa hakuna lami licha ya kuongozwa na Serikali ya Chama tawala (CCM).


Mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Jimbo la Mbozi Ester Kayombo amewataka wanawake wenzake na wananchi kwa ujumla kuungana kupigania haki na maslahi yao kwa madai kuwa CCM inajinufaisha yenyewe na wachache.


"Acheni kuiogopa CCM, CCM haiwalishi wanaonufaika na CCM ni wachache wako huko juu, ukisema wewe ni mwana CCM uko huku chini unajidanganya, wamekupa nini zaidi ya kusubiri kipindi cha uchaguzi wakupe t-shirt na kitenge si wanawake wenzangu mnajihangaikia kwa kuuza mbogamboga hapa Isansa, kuuza nyanya na kulima", ameeleza Mwenyekiti wa BAWACHA jimbo la Mbozi akizungumza na mamia ya wanachama na wananchi katika kata ya Isansa Mbozi Mkoani Songwe.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI