Header Ads Widget

MDUDE NYAGALI AITUHUMU SERIKALI KULEA WIZI, ADAI DENI LA TAIFA LIMEFIKIA TRILLION 100.

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania Mdude Nyagali Mpaluka amesema uongozi wa Serikali ya Tanzania umechoka ndio maana maisha ya wananchi yanaendelea kuwa magumu kwa viongozi kushindwa kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao.


Mdude ambaye ni muambata wa sauti ya wa-Tanzania na mfuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, ameeleza hayo wakati akizungumza na mamia ya wananchi katika kata ya Mpuguso huko Ushirika Tukuyu Wilayani Rungwe ambako amekemea masuala kadhaa ikiwemo kutosimamiwa vizuri kwa raslimali za Taifa, kupanda kwa gharama za maisha, Serikali kutoruhusu kupatikana kwa katiba mpya na mengineyo mengi.


Pia mwanaharakati huyo wa masuala ya haki za binadamu, amesema ni ajabu Serikali kuendelea kukopa fedha ambazo sasa zinafikia trillion mia moja lakini haionekani zikileta tija kwa wananchi kiasi kwamba zinafujwa na viongozi Serikalini.


Mdude amewataka wananchi kwenda kuichagua CHADEMA kwenye chaguzi zijazo ili kuleta mabadiliko ya kweli.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Kanda ya Nyasa Tabia Mwakikuti amewataka wanawake wa CHADEMA wenye nia na uwezo kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Serikali za mitaa hadi uchaguzi mkuu.


Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Rungwe Gideon Mwakila amewaomba wananchi wa Jimbo la Rungwe kwenda kuiamini CHADEMA kwenye uchaguzi ujao kwa kuwachagua wagombea wake.


Kwenye mkutano huo wa hadhara wa CHADEMA na wananchi, katika hali isiyo ya kuzoeleka, Diwani wa kata ya Mpuguso Rungwe Mhe. Japhet Mwakagugu (CCM) amehudhuria na kusema wapinzani wanapokosoa CCM itaendelea kurekebisha kwa maendeleo zaidi na siasa sio ugomvi.


CHADEMA kinaendelea na mikutano ya kuimarisha umoja na mshkamano ndani ya Chama hicho na kuwaandaa wananchi kwa ajili ya chaguzi zijazo kikiendelea kueleza sera zake ili kuchaguliwa kwenye chaguzi zijazo.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI