Serikali imeridhia ombi la kuondoa ushuru wa shilingi 382 iliyokuwa imepanga kuweka kwenye kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari kuanzia mwaka ujao wa fedha (2024/2025).
Ushuru huo umeondolewa kufuatia ushauri wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti chini ya mwenyekiti wake Mhe. Oran Njeza ambayo imeeleza kutokubaliana na ushuru huo kwani sekta ya gesi bado ni changa na inaendelea kukua taratibu na hadi sasa haijatumika kikamilifu nchini kutokana na gharama za kufunga mfumo wa kutumia gesi pamoja na uhaba wa vituo vya kujazia gesi.
Wabunge wengi waliochangia hotuba ya bajeti ya Serikali 2024/2025 walipinga kuanzishwa kwa ushuru huo wakisema kuwa unaenda kinyume na azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuchagiza matumizi ya nishati safi nchini.
Katika uwasilishaji mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya bajeti Mhe. Oran Manase Njeza amesema kamati yake imeishauri Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumika kuunganisha mfumo wa gesi ili kupunguza gharama za kusimika mfumo huo kwenye magari ambazo kwa sasa gharama za ufungaji zinakadiriwa kuwa kati ya shilingi Milioni mbili na Milioni tatu, kiwango ambacho kinaelezwa kuwa ni kikubwa.
0 Comments