Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa wilaya Kigoma Salum Kali amewataka wananchi wa mkoa Kigoma kukemea kauli na mienendo inayoashiria kuwagawa watanzania na kupandikiza chuki baina yao huku akiwataka kuhubiri amani na upendo kwa watu wote.
Kali ametoa kauli hiyo leo mjini Kigoma wakati akitoa salam kwenye sala ya Eid AL adha ambayo kimkoa imefanyika kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini Kigoma na kusema kuwa mawaidha ya viongozi wa dini yawaongoze watu wote katika Maisha yao ya kila siku.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kutokana na maono na misingi iliyowekwa na viongozi wake ambao wameitunza na kuidumisha amani hiyo kwa muda mrefu ambapo amesema kuwa wakati huu kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu watanzania wameaswa kuacha kufanya siasa za chuki.
Alibainisha kuwa uwepo wa amani nchini imekuwa nguzo kubwa ambayo imeifanya serikali chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan kutumia mabilioni ya shilingi katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Shekhe wa mkoa Kigoma,Hassan Kiburwa Shekhe wa kata za Mwanga manispaa ya Kigoma Ujiji, Ismail Nassoro alisema kuwa Eid Al Adhaa inawakumbusha waumin wa kiislam kufuata mafundisho ya dini yao kama alivyofanya Nabii Ibrahim ambaye alielekezwa kumchinja mtoto wake ambapo hata hivyo Mwenyezi Mungu alimshushia mnyama badala ya kumchinja mwanaye.
Alisema kuwa waumini wa kiislam wakifuata mafundisho na maelekezo ya dini wataishi kwa upendo, amani na mshikamano na kutaka waislam kusaidiana kwa hali na mali pale mmoja wao anapopatwa na shida.
Mwisho,
0 Comments