Header Ads Widget

ASKOFU MKUU DKT. MTOKAMBALI AITAKA TUME YA UCHAGUZI KUEPUKA UBAGUZI CHAGUZI ZIJAZO.

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Askofu mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Mch. Dkt. Barnabas W. Mtokambali, amezitaka mamlaka nchini Tanzania ikiwemo Tume ya uchaguzi na Jeshi la Polisi kusimamia haki kwenye chaguzi zijazo ili kudumisha upendo na amani ya Taifa.


Askofu mkuu huyo, ametoa rai hiyo wakati wa mahojiano yake maalum kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani nchini Tanzania.

Dkt. Mtokambali ambaye pia ni Rais wa kanisa hilo barani Afrika na mjumbe wa kanisa la Assemblies of God (AG) Duniani, amewataka wananchi kujitokeza kuhuisha na kuandikisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali kwenye chaguzi hizo ili kupata viongozi waadilifu katika kuwaletea wa-Tanzania maendeleo.


Ameishauri Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania (INEC) kusimamia na kutenda haki kabla, wakati na baada ya chaguzi ili wananchi kupata fursa ya kushiriki chaguzi hizo kwa kuchagua viongozi wanaowataka ili kuepuka upendeleo.

Kiongozi huyo mkuu kanisa la TAG nchini amesema Tume ya uchaguzi haitakiwi kuruhusu aina yoyote ya ubaguzi ili kuendelea kuhifadhi umoja wa kitaifa.


"Na nitoe wito pia kwa tume ya Taifa ya uchaguzi kwamba katika ngazi zote isimamie uchaguzi huu kwa uadilifu, kwa kufuata sheria, kanuni na kufuata taratibu zote za nchi bila kuleta upendeleo au ubaguzi wa aina yoyote kwasababu hali ndio msingi wa kuliinua Taifa, utulivu na amani ya Taifa", amesema Dkt. Barnabas Mtokambali, askofu mkuu wa TAG.

Aidha kiongozi huyo amevitaka vyombo vya dola kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuongeza umakini kuelekea chaguzi za kiserikali ili kutoruhusu maadui wa ndani na nje ya nchi kujipenyeza na kuharibu amani ya Taifa.


Augustino Luvanda ni mkazi wa jijini Mbeya, anasema huu ni wakati wa wananchi kuendelea kuwapima wanasiasa kwani wengi wamekuwa na maneno mazuri lakini baadaye wanageuka kuwa wapenda Rushwa na wenye kufanya kazi kwa maslahi binafsi huku Bi. Irene Dickson na Keneth Manamba wakisema lazima waendelee kumwomba Mungu ili awape viongozi sahihi badala ya kurubuniwa na wanasiasa wasio Wazalendo hivyo kupata viongozi wasio na sifa.


Askofu mkuu wa kanisa la TAG nchini Tanzania Mchungaji Dkt. Barnabas Weston Mtokambali, anatoa maoni na mwito wake kwa Taifa juu ya masuala ya chaguzi ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa kote nchini (Tanzania) ambao unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu (2024) huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika Oktoba 2025 ambapo wananchi hawana budi kuendelea kujiandaa kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha na kujiandikisha majina yao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambayo ni haki yao kikatiba kuchaguliwa na kuchagua viongozi wanaowataka.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI