Wasimamizi wa rasilimali za bahari na utunzaji wa mazingira (BMU) kwa kushirikiana na Wananchi wilayani Kigamboni wameandaa kongamano la kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri katika kuwatumikia wananchi hususani katika fulsa kwenye sekta ya uchumi wa bluu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kigamboni jijini Dar es salaam Mratibu wa kongamano Omari Rajabu Kombe amesema kongamano hilo la siku mbili tarehe 29- 30 mwezi huu litaonyesha shughuli mbalimbali zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita ikiwa ni pamoja na walionufaika na mikopo kwa wavuvi, shughuli za sekta ya utalii, ufanyaji wa usafi katika fukwe za maeneo ya mji Mwema wilayani Kigamboni.
Amesema shughuli zingine zitakazofanyika ni pamoja na Tamasha la michezo watakaohudhuria ikiwa ni pamoja na michezo ya mashindano ya ngalawa baharini, kuogelea, lede, kukuna nazi, kuvuta kamba na Beach soka.
Amesema siku ya uzinduzi saa za alfajiri siku ya tarehe 29 mwezi huu kongamano hilo litaanza kwa matembezi ya fukwe kwa fukwe kwa ushirikiano wa vikundi vya vijana wa Jogging kutoka wilaya za Kigamboni, Temeke, ilala, kinondoni na Ubungo ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo na Mgeni maalumu anatarajia kuwa Mkurugenzi wa Clouds Media Joseph Kusaga.
Omari amesema kongamano hilo linatarajia kufungwa tarehe 30 mwezi huu na Mgeni rasmi anatarajia kuwa Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Aidha ameyataja mashirika mbalimbali yatakayotarajia kushiriki kongamano hilo kuwa ni TAFICO, TASAC, Marine pack reserve, TRA, CRDB, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya Kigamboni.
Naye mjumbe wa kamati mipango na fedha Sofia Mjasili ameomba Msaada na ushirikiano wa Hali na mali kutoka kwa Wadau mbalimbali kufanikisha kongamano hilo.
Sofia amesema taasisi ya Wanawake na Samia pia itashiriki katika kongamano hiyo kwani wanamtakia mema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Uongozi wake.
0 Comments