Na Matukio Daima App Buchosa
MUNGU wetu yu mwema, kila wakati na daima fadhili zake ni za milele.
Waraka au barua hii nzito, ni mjumuisho, mkusanyiko, mrundikano, muungano na ushiriki wa mawazo yenye maana na ujumbe mmoja, kutoka kwa wakazi na wananchi wengi wa Jimbo na Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Binafsi, kama Mwandishi wa Habari kitaaluma na maisha, wajibu wangu ni kuitumia vyema kalamu yangu kuwasilisha na kuweka kumbukumbu sawa.
Naomba niweke bayana jambo moja muhimu na lipewe nafasi kubwa kwa Kila atayesoma barua hii kuwa, sijawahi na kamwe siwezi kutumia kalamu yangu vibaya kwa lengo na dhamira ya kumshambulia na kumuumiza mtu, ama kwa kutumika au kwa matakwa binafsi, kamwe siwezi.
Wakati napokea wito kutoka wa wananchi wenzangu mbalimbali wa maeneo tofauti tofauti ya Jimbo la Buchosa, wakiniomba na kunitaka niandike barua hii kwa niaba yao, ilinilazimu nijipe muda wa kutosha, kufanya uchunguzi, ufuatiliaji na kujiridhisha pasina shaka, juu ya madai na malalamiko yao!
Miito ya simu ilikuwa mingi. Milio ya jumbe (SMS), zilikuwa za kutosha, madai na malalamiko yakiwa na maudhui yaleyale!
MSINGI WA MADAI!
Malalamiko yaliyotajwa kwa uchungu na hisia kali, tena walalamikaji wengi wakiwa wazee na wengine wenye umri wa kati, yalinifikirisha na kunihuzunisha sana.
CHOKOCHOKO, UCHOKOZI NA FUJO ZA DKT. TIZEBA KWA MBUNGE SHIGONGO!
Haya ndiyo yalikuwa madai ya mamia, maelfu na makundi mbalimbali ya wananchi wa Buchosa!
Madai ya wakazi wa Buchosa, ni kuwa aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Charles John Tizeba, anafanya fujo, fitina na vita za kisiasa, akiwa na lengo la kuhujumu juhudi za Mhe. Eric Shigongo, akitumia kila njia na hila za kumchonganisha mbunge Mhe. Shigongo kwa wananchi!
Madai yalienda mbele zaidi, ikielezwa kuwa fujo za kisiasa za Tizeba zilianza tangu kushindwa kwake katika nafasi ya ubunge na Mhe. Eric Shigongo James, tangu 2020.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, nilifunga safari hadi jimboni Buchosa, ili kufanya uchunguzi na ufuatiliaji wa kina, juu ya jambo hili zito!
Katika utafiti wangu, tena nikitumia elimu, taaluma, weledi, maadili ya uandishi wa habari na akili ya kuzaliwa, nilibaini na kugundua kuwa ni kweli tuhuma hizo dhidi ya Tizeba, za kumfanyia fujo na fitina Mbunge, Mhe. Eric Shigongo, ni za kweli huku nikipata na zingine zaidi, nje ya malalamiko ya awali!
KWAKO SASA DKT. TIZEBA!
Niweke kumbukumbu sawa. Mimi ni mwenyeji wa Jimbo la Buchosa, familia yangu, ipo Buchosa.
Kwetu ni Kata ya Iligamba, Kijiji cha Chang'ombe, mtaa wa Mawenzi. Hivyo, ninaifahamu Buchosa.
Dkt. Tizeba, unanifahamu vyema mzee wangu. Hata nilipopata malalamiko haya, nilikutafuta. Wewe ni shahidi katika hili.
Tizeba, nilikuwepo Buchosa mwaka 2010, wakati mnagombea pamoja na Mhe. Shigongo, pamoja na wagombea wengine.
Nawakumbuka akina Jowa, Dkt. Sengati, Chitarilo na Makanza. Kama una kumbukumbu nzuri, hata kwenye mchakato wa kura za maoni, kuna fujo ulizifanya, ambazo nitaziweka wazi katika sehemu ya pili ya barua hii kwako, Kuna kumbukumbu bado nazikusanya za fujo ulizikuwa ukimfanyia Shigongo.
Tukio moja ninalolikumbuka, ni kumpelekea watu wa Takukuru nyumbani kwake, kwa uongo na fitina za madai ya rushwa! Kitu ambacho kilikuwa UONGO MKUBWA!
Sehemu ya pili, nitaelezea mazingira yote kwa kina!
Baada tu ya kumalizika kwa mchakato huo, nakumbuka Mhe. Shigongo aliondoka kabisa Buchosa, lakini aliacha ujumbe bora na muhimu kwa wananchi wa Buchosa, akiwaomba waungane na wewe kupambana, ili ushinde na kukiweka madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa ushawishi mkubwa aliokuwa nao wakati wa mchakato, Mhe. Shigongo endapo angeamua kugomea matokeo, sura ingekuwa nyingine Buchosa!
Lakini kwa hekima, busara, nidhamu binafsi, upendo wake kwa wana Buchosa na kwa hofu ya Mungu, Mhe. Shigongo alikubali yaishe.
Katika kipindi chote cha ubunge wako, kuanzia awamu ya kwanza, Ile miaka mitano, Shigongo hakuwahi kukusumbua kwa lolote!
Mwaka 2015, hakuthubutu, kuwaza wala kujaribu kugombea, alikuacha ukamilishe yale ambayo hukuyamaliza kuyatimiza katika kipindi chako cha kwanza.
Shigongo alikuheshimu, hakuwahi kukanyaga Buchosa kwa lengo la kukufanyia fitina wala fujo ya aina yoyote, zaidi ya kwenda mapumziko ya Kila mwisho wa mwaka (maana ndiyo nyumbani kwake, wakati mwingine kwa mambo ya kifamilia).
Tizeba, kwa nini wewe umekuwa mtu wa kumfanyia fujo mwenzio wakati akitekeleza majukumu yake mazito ya kuzisemea shida za wananchi kwa Serikali?
Kwa nini Tizeba unakuwa mtu tena bingwa wa kuchochea majungu kwa wananchi? Mbona mwenzio alikuheshimu? Au uliamini anakuogopa sana?
Unamjua vizuri Shigongo? Siku kiwango cha kukuvumilia kikimfikia mwisho, nakuonea huruma kwa machozi mazito! Namjua!
Mbaya zaidi, hata wakati ukiwa mbunge, yeye akiendelea na maisha yake mengine, wewe uliendelea kumtukana kwa maneno ya fedheha, tena ukiweka ukabila mbele!!!!!!
Wewe ni msomi wa aina gani? Hizo degree tatu ni za aina gani? Umeliacha Jimbo la Buchosa likiwa limetawaliwa na chuki za kikabila, ulizozipandikiza wewe na genge lako!
Kazi ya kwanza ya Shigongo baada ya kuingia madarakani, ilikuwa ni kuondoa sumu kali ambayo ulifanikiwa kuipandikiza kwa maeneo mengi Buchosa.
Badala ya kuanza kushughulikia kero na matatizo ya wananchi, ikamlazimu Mhe. Shigongo atumie muda mwingi kuhubiri umoja, mshikamano na umoja, unaona hasara ya muda uliyompa mwenzio?
Mbona wewe Chitarilo hakukufanyia hivyo wakati akiwa mbunge?
Nimeenda maeneo mengi ya Buchosa, kila kona wananchi wanashuhudia jitihada za Mhe. Shigongo. wanaona mambo anayoyafanya, wanamuona anavyohangaika ndani na nje ya Bunge akiwapigania usiku na mchana, lakini wanalalamika unavyomfanyia fujo!
Barua hii, ni lazima isomwe na wananchi wote wa Buchosa, kupitia sinema. Itawekewa sauti, Kila mwana Buchosa aisome kwa njia ya sauti.
Nitapita jimbo zima kuwasomea wananchi, wakujue jinsi ambavyo hauna nia njema na Jimbo la Buchosa, zaidi ya maslahi yako binafsi!
Mwishoni mwa mwaka jana, nilikuwa Buchosa. Mhe. Shigongo, kama Mbunge husika aliamua kwa nia njema tu, asherehekee sikukuu pamoja na wananchi, wakiwemo viongozi wa Chama na Serikali.
Lakini cha ajabu, ukawazuia baadhi ya wanachama, ukaandaa sherehe ya maksudi tu huko kwenu Kome, ukagawa vitu mbalimbali, lengo tu uharibu lengo la Mbunge kula sikuuu na wananchi, pamoja na viongozi.
Kama mwananchi, nilikuwepo nyumbani kwa Mhe. Shigongo. Alizungumza mambo mengi ya kimaendeo, ikiwemo kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini kwetu.
Tizeba wewe ni mtu wa fujo sana! Huna maelewano mpaka na ndugu zako, kisa ubinafsi na majungu!
Unakumbuka siku tulipokutana kwenye ferry Kamanga?
Unakumbuka ulijiapiza nini kuhusu Shigongo? Sehemu ya pili ya Barua hii, nitaweka wazi kila kitu, labda uape kuwa umekoma kufanya fujo zako na tabia ya majungu na chuki utaiacha!
Nikiwa namalizia sehemu hii ya kwanza, nitoe rai, ombi na wito kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ngazi ya wilaya na mkoa, muiteni Tizeba na mumuonye anamharibia mwenzake.
Siyo utaratibu wa CCM kufanya matendo anayoyafanya Tizeba Jimbo Buchosa.
Hata hivyo, ni bahati tu kwamba Mhe. Shigongo ni muungwana na muumini mkubwa wa AMANI, vinginevyo kwa vimbwanga anavyovifanya Tizeba, hata mashati wangekuwa wameshakunjana!
Kama mmewahi kumuonya, basi bado anaendelea.
Kama hamkuwa mkijua, basi ukweli ni kwamba, Tizeba anamfanyia fujo Mbunge Shigongo! Anzeni kuchunguza!
Sababu kubwa inayomfanya Tizeba aumie, ni kwamba mambo ambayo ameyafanya Shigongo katika kipindi hiki cha kuelekea miaka minne ya ubunge wake, ni makubwa zaidi ya alichokifanya Tizeba kwa MIAKA 10 yote akiwa Mbunge, tena waziri.
Pia, niweke sawa jambo moja. Sijatumwa na mwanasiasa yoyote kuandika barua hii, zaidi ya wananchi wanaoumia kuona mtu anayewatetea na kuwaletea maendeleo (Shigongo) akifanyiwa fujo na Tizeba.
Mimi kama Mwandishi, siwezi kufumbia macho. Ni kweli nafahamiana na Shigongo, kama ambavyo pia nafahamiana na Tizeba. Wote ni jamaa zangu, lakini yoyote kati yao akienda tofauti na utaratibu, kalamu yangu ni lazima imwage wino kama hivi.
Sehemu ya pili ya barua hii, nitaelezea kwa ukubwa mambo makubwa yaliyofanyika Buchosa katika kipindi cha ubunge wa Shigongo hadi sasa, nikilinganisha na alichokifanya Tizeba.
Imetosha kwa leo. Imeandikwa na mwananchi wa Jimbo la Buchosa, ambaye pia ni Mwandishi wa Habari kitaaluma.






0 Comments