Na Ashton Balaigwa,MOROGORO
BALOZI wa Ubelgiji nchini Tanzania,Peter Van Acker amesema kuwa nchi yake inajivunia kuwa na ushirikiano mzuri na Serikali ya Tanzania kwa miaka 40 katika kufanikisha kwenye nyanja ya uchumi,afya,maji na elimu kwamba itaendelea kudumisha Diplomasia pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kusimamia uwiano wa jinsia na Demokrasia na Utawala bora.
Balozi Van Acker amesema mafanikio hayo yanatokana na Umoja wa Vyuo vikuu vya nchini Ubelgiji na Chuo Kikuu Mzumbe(MU) kilichopo Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro kuwa na ushirikiano kwa kipindi cha miaka 10 katika utekelezaji wa Program za kitaaluma kwa kufanya utafiti na kuzitatufitia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye jamii,elimu ya ujasiriamali na upatikanaji wa huduma ya maji safi.
Balozi huyo wa Ubelgiji nchini Tanzania, alisema hayo kwenye hafla ya kufunga program hiyo ya miaka 10 iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikalini na uongozi wa chuo kikuu cha Mzumbe.
Alisema kuwa nchi yake kupitia ushirikiano wa tafiti mbalimbali imesaidia serikali ya Tanzania katika mipango yake ya kusaidia kwenye nyanja za kiuchumi,afya,maji na elimu kupitia miradi mbalimbali waliofadhili
”Kukamilika kwa pragramu hii siyo mwisho bali ushirikiano kati chuo kikuu cha Mzumbe na Ubelgiji katika masuala ya kitaaluma utaendelea kwa kutoa ufadhili katika kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia jamii kwenye maendeleo yao.”alisema Balozi huyo.
Akifunga program hiyo,Mkuu wa wilaya ya Mvomero Judith Nguli, kwa niaba ya Mkuuwa Mkoa wa Morogoro Adam Kigoma Malima,alipongeza jitihada zinazofanywa na Ubelgiji katika kusaidia program hiyo ya kufanya utafiti wa masuala ya kitaaluma na kijamii na kutaka uendelee katika Wilaya nyingine za mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa wilaya aliutaka uongozi wa Mzumbe kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya demokrasia na utawala bora kwa viongozi wa serikali za mitaa waliopo madarakani na wale ambao watakaochaguliwa katika uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Alisema kuwa kazi inafanywa na chuo kikuu cha Mzumbe ni kubwa na serikali ina matumaini makubwa na chuo hicho katika kusaidia kutoa maarifa na ujuzi katika masuala ya uongozi kwa watu.
Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Mzumbe Profesa William Mwegoha alisema kuwa mradi huo ambao unatekelezwa na umoja wa Vyuo vilivyopo Ubelgiji umekuwa na manufaa makubwa kwa chuo cha Mzumbe na serikali kwa ujumla.
Profesa Mwegoha alisema moja ya mafanikio hayo ni pamoja na kupanuka kitaaluma kwa wanataaluma 12 kuhitimu shahada za uzamivu kwa kufanikisha malengo ya kimkakati ya chuo katika masuala ya Tehama katika kutengeneza mitaala na kuboresha njia ya ufundishaji.
Alitaja maeneo mengine ambayo yameleta tija kupitia mradi huo ni kuwa na wataalamu wenye ubobezi kwenye ubunifu katika ufundishaji na kuwa tija kwa chuo na jamii kwa ujumla.
Mbali na eneo la kitaaluma pia amebainisha ya kuwa wananchi wa mvomero wamenufaika katika kupata ujuzi kwenye masuala ya ujasiriamali na kubuni teknolojia ya maji na ubora wa maji kwenye vijiji 15 vilivyopo katika Wilaya ya Mvomero
0 Comments