NA WILLIUM PAUL, HAI.
SERIKALI imelipa fidia ya Bilioni 11.5 kwa wananchi wa kaya 1061 ambao walivamia katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) waliokuwa wameweka makazi ambapo wameanza kuvunja makazi yao na kupisha eneo hilo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Kilimanjaro ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Nurdin Babu ilifika katika maeneo hayo na kushuhudia jinsi wananchi wakivunja makazi yao wenyewe na kuhaka ambapo wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa busara aliochukua kuwaalipa ilihali wao ndio wamevamia katika eneo la uwanja.
Akizungumza Diwani wa kata ya Kia, Tehera Mollel alisema kuwa kazi ya kuwahamisha Wananchi waliovamia katika eneo la uwanja na kuweka makazi ilifanyika kwa uaminifu mkubwa ambapo Wananchi wameridhika na fidia waliyopewa.
Diwani huyo alisema kuwa, mara baada ya kulipwa fidia hiyo wananchi waliamua kuhama wenyewe ambapo kwa sasa lipo greda ambalo hupita na kuvunja magofu yaliyopo katika maeneo hayo kusafisa eneo hilo baada ya wananchi kuhama wenyewe.
“Hakuna Mwananchi wa Kia ambaye amebomolewa nyumba kama inavyoenezwa katika mitambao ya kijamii sisi tumevunja wenyewe na ni baada ya kufanyiwa tathimini na kulipwa fidia ambapo tumeweza kwenda kujenga makazi mengine katika maeneo sahihi” alisema Mollel.
Alisema kuwa, Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa ajili ya wananchi kuhama baada ya kulipwa fidia ambapo ilitoa fursa kwa wananchi kujiandaa hali ambayo imepelekea wananchi kwa hiari yao wenyewe kuvunja nyumba zao na kukanusha kuwa hakuna uharibifu wowote uliofanyika katika zoezi hilo.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Loktoli, Daud Sokoine alisema kuwa, serikali ilifanya tathimini awali na hakuna mtu yeyote aliyeachwa na baadha ya tathimini hiyo serikali imelipa fidia ambapo imewawezesha wananchi kujenga nyumba katika maeneo mengine.
“Ikiwa eneo sio la kwako na umevamia na kujenga makazi kwa mujibu wa taratibu kama hili la serikali lakini bado ikaona ipo haja ya kutulipa fidia hili ni jambo la kiungwana na la kupongeza sana ikiwa umeingia kwa mtu bila utaratibu akaja akakuondoa na bado akakupa nauli ni jambo la kushukuru” alisema Sokoine.
Alisema kuwa, zoezi la kuvunja mapagale ambalo limekuwa likifanyika kwa sasa bado limekuwa likifanyika kwa buisara kubwa ambapo pia wananchi wamaekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa na kuomba Serikali kufikisha huduma katika maeneo ya pembezoni walipoamia na kujenga makazi ikiwemo umeme na maji.
Mara baada ya kusikiliza Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa, wananchi hao walivamia katika eneo hilo la uwanja wa ndege na kujenga makazi lakini kwa sasa linahitajika kwa ajili ya matumizi mengine.
Babu alisema kuwa, serikali iliamua kutumia busara kuwalipa wananchi hao fidia ya Bilioni 11.5 kwa wananchi wa wilaya ya Hai pamoja na Arumeru ili kupisha eneo hilo ambapo waliamua kuvunja nyumba zao wenyewe na kupisha eneo hilo.
“Hakuna mwananchi ambaye ameondoka katika eneo hili bila kulipwa fidia hivyo nawaombeni Wananchi mumuonee huruma Rais kunawatu wengi wao kila kinachofanyika na serikali kwao ni kibaya hawataki lakini tambueni Serikali inaubinadamu na utu na inajali haki zote za binadamu na ndio maana zoezi hili tumeshirikishana mwanzo mwisho” alisema Babu.
Alisema kuwa, awali wananchi hao bila kutambua walivamia eneo hilo ambalo ni mali ya serikali na kuweka makazi ambapo serikali imeamua kutumia busara kuwalipa fidia ili kuondoka kupisha eneo hilo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Hai, Amir Mkalipa alisema kuwa, zipo nyumba kadhaa ambazo hazikulipwa fidia kutokana na sababu mbalimbali ambapo wameweza kurekebisha makosa yao na sasa wameshaingiziwa fedha za fidia jana.
Mkalipa alisema kuwa, asilimia 95 ya wananchi wameshahama katika eneo hilo ambapo kwa sasa wanachofanya ni kusafisa eneo hilo kwa kuondoa mapagale baada ya wananchi kuhama wenyewe kwa hiari yao.
“Zoezi la kuondoa pagale limeenda kwa ufanisi mkubwa na hakuna uharibifu wala uonevu uliofanyika na wala hakuna nyumba ambayo imevunjwa bali kinachofanyika ni kuvunja mapagale baada ya wananchi kuhama” alisema Mkalipa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, Wananchi walipaswa kuhama katika kijiji cha Sanya stesheni ni ni kaya 596, kijiji cha tindigani kaya 402, kijiji cha Chemka kaya 62, ambapo jumla ya kaya 1061 zilizolipwa fidia kwa ajili ya kuhama.
0 Comments