Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Adam Malima amesema Ujio wa Reli ya kisasa ya Treni ya mwendo Kasi, SGR, utafungua zaidi fursa za kiutalii kwa mkoa huo ambapo Serikali imejipanga kuweka geti jingine la kuingilia Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kutokea stesheni ya Reli ya Kilosa ili kutoa fursa Kwa watalii kuchagua njia yeyote kufika hifadhini.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za utalii kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Morogoro yaliyokuwa yakitolewa na wakufunzi kutoka chuo cha Taifa cha utalii.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na chama cha waandishi wa habari Tanzania, TAMPA, kwa ufadhili wa shirika la hifadhi za Taifa TANAPA.
Mkuu huyo wa Mkoa akataka waandishi hao kuandika habari sio tu za kuvutia wawekezaji bali pia zitakazovutia wawekezaji kuwekeza katika Sekta ya Utalii ili idadi ya watalii ikiongezeka wapate na maeneo ya kulala, kula na kufanya shughuli zao za utalii vizuri.
Aidha akasema waangalie uwekezaji unaoendelea kama unakidhi vigezo na ubora na kuhimiza ushindani huo ulenge kujipima na masoko mengine duniani.
"Mfano kuna hoteli moja Mikumi nilifika nikawa naulizia msalani, wale wahusika wakaja mbio kuniomba Radhi nisiingie, waniandalie chumba kimoja maalum,nikakataa nikasema hapana,nakwenda huko huko wanakokwenda wengine, nilipofika nilijuta, hata sikuweza kuingia, sasa kwa namna hii huwezi mshawishi mtalii akafikia kwako, lazima tuwe tunakagua na haya mazingira ni kweli wawekezaji wanazingatia ubora na vigezo"Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Akasema wamejipanga kuufanya mji wa Mikumi kuwa mji wa Kitalii na kuhimiza wanahabari wa Mkoa wa Morogoro kuandika habari za vivutio vilivyopo,upekee wake na namna ya kuvifikia.
"Waambieni kuna hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa, Nyerere, bonde la Kilombero, mimea na wanyama wasiopatikana kwingineko duniani, Misitu,historia na mambo ya kale na vivutio vingine vingi, Mfano bonde la Kilombero katika hifadhi ya Nyerere kuna samaki anaitwa Tiger Fish, watalii wamekuwa wanakuja kumvua na kucheza naye, lakini huenda Sisi (watanzania)hatujui"Aliongeza.
Akaagiza kundi hilo la waliopata mafunzo kuwa kamati maalum ya kuhamasisha shughuli za kiutalii za Mkoa wa Morogoro na kwa kuanza watatembelea hifadhi za Mikumi, Udzungwa na Wami Mbiki walio chini ya Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini TAWA, pamoja na kuangalia fursa zingine zaidi zilizopo.
Mapema Rais wa TAMPA Bw.Simon Mkina, alisema mafunzo hayo yaliandaliwa maalum kuwawezesha waandishi wa habari kufahamu fursa mbalimbali zilizopo kwenye Sekta ya Utalii na kujua namna bora ya kuziandika ili kuvutia wageni wengi kufika kujionea.
Akasema mafunzo hayo tayari yameshafanywa kwa mkoa wa Dar es salaam na yataendelea kwa mikoa mingine kote nchini.
Akawataka wanahabari hao sio kuutangaza mkoa wa Morogoro kiutalii Peke, Bali popote watakapoweza kufika wafanye hivyo na chama hicho kitakuwa tayari kuwasaidia kwa kuzingatia masharti na vigezo.
Naye Katibu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Morogoro Bi Lilian Lucas akaahidi waandishi hao wa habari watakuwa mabalozi wazuri wa Sekta ya utalii.
Tanzania imekuwa ikipokea wastani wa watalii Milioni moja na nusu kila mwaka, lakini malengo ya Serikali kwa sasa ni kufikisha watalii Milioni tano.
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imekuwa ni rahisi kufikika kirahisi kwa magari kutoka na kuwa ya kipekee kupitwa na barabara ya lami katikati ya Hifadhi hadi lango kuu, pamoja na ndege, baada ya kukarabati uwanja wake wa ndege ulio ndani ya Hifadhi ambapo makundi ya watalii yamekuwa yakiingia na kutoka kila siku.
Hata hivyo Malima alisema wanatamani kuona watalii hao wakija wanabaki baada ya kuboreshwa na kuongezwa uwekezaji ukiwemo ujenzi wa hoteli za kisasa zenye viwango vya juu kumvutia mgeni.
Aidha wakufunzi kutoka chuo cha Taifa cha utalii Amiri Abdi na Lasway Agapiti walisema utalii sio wa wanyama pekee Bali yapo maeneo mengi yakuvutia watalii ikiwemo utalii wa matibabu, Mila na desturi, mambo ya kale, maporomoko ya maji,Majengo, vitu vya asili na maeneo mengine mengi ambayo wanahabari wanaweza kuwaeleza wadau wa utalii wakiwemo watalii wenyewe.
0 Comments