Header Ads Widget

WANANCHI SONGWE KUNUFAIKA NA MADAKTARI BINGWA NA BOBEZI 25 WA KAMBI YA SAMIA.

MKUU WA MKOA WA SONGWE DANIEL CHONGOLO

Na Moses Ng’wat, Matukio Daima App Songwe.


WANANCHI wa Mkoa wa songwe wanatarajia kunufaika na huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ambao watapiga kambi ya siku tano katika Hospitali za Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe kwa siku tano.


Matarajio hayo yamebainishwa leo Mei 13, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, wakati wa mapokezi ya madaktari hao bingwa na bobezi 25 kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo watapiga kambi ya siku tano na kutoa matibabu ya kibingwa na bobezi kwa wagonjwa mbalimbali.


Chongolo alisema kufanyika kwa kambi hiyo (maarufu kama kambi ya matibabu ya Rais Samia) ni sehemu ya mpango wa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kusogeza huduma za matibabu hasa ya kibingwa ambayo watu wengi wanahitaji lakini hawapati fursa ya kuyapata kutokana na kutokuwepo kwa madaktari bingwa wa fani hizo na kushindwa gharama ya kufuata huduma hizo nje ya Mkoa wa Songwe.


“Wananchi wa Mkoa wa Songwe tuna mategemeo makubwa si ya kupata matibabu tuu bali tunaomba pia mrithishe ujuzi na uzoefu wenu bobezi wa kutoa matibabu na huduma za afya kwa wataalam wetu huko mnakoenda kufanya kazi katika Wilaya zetu” alisisitiza Chongolo. 


KIONGOZI WA TIMU YA MADAKTARI BINGWA DKT AANA MAGEMBE 


Kiongozi wa timu ya madaktari hao bingwa na bobezi, Dkt.Anna Magembe ambaye ni daktari bingwa wa watoto na bobezi wa matatizo ya damu na saratani kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, alisema ujio wa madaktari hao bingwa watahusika kutoa huduma katika maeneo makuu matano.


Aliyataja maeneo hayo kuwa ni madaktari bingwa wa watoto, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Upasuaji, wanawake na uzazi, wakiwemo madaktari bingwa wa usingizi na ganzi.


Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu, alisema ujio wa madakatari hao ubingwa utawanufaisha wananchi kwa kiasi kikubwa kutokana na mkoa huo kukabiliwa na changamoto ya  kukosa madaktari bobezi.


Alitaja maeneo hayo yaliyokuwa na changamoto kuwa ni kukosa madaktari bingwa na bobezi kwenye eneo la huduma za afya ya uzazi na mtoto, magonjwa ya ndani, pamoja na ukosefu wa daktari bingwa na bobezi wa upasuaji hali ambayo ililazimu wagonjwa wengi kupewa rufaa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI