Header Ads Widget

TIMU YA MADAKTARI BINGWA 40 WAWEKA KAMBI SINGIDA

TIMU YA MADAKTARI BINGWA 40 WAKIWA MKOANI SINGIDA


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 


MADAKTARI Bingwa 40 wameweka kambi ya siku saba katika Mkoa wa Singida kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi katika hospitali  zote za wilaya zilizopo mkoani hapa.


Afisa Programu kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, Joachim Masunga,akizungumza jana wakati wa kuwatambulisha madaktari hao kwa uongozi wa Mkoa wa Singida, amesema madaktari hao watatoa huduma mbalimbali zikiwamo za upasuaji.


Amesema lengo kubwa la madaktari kutoa huduma za kibingwa ni kuwapunguzia wananchi mzigo wa kufuata matibabu sehemu nyingine na kutumia gharama kubwa na sasa watapata huduma hizo katika maeneo yao.


"Kama ilivyo kauli ya kwamba Mama anamtua mwanamke ndoo kichwani na sisi kwa upande wa afya tunataka kuwapunguzia mzigo wananchi kufuata huduma za kibingwa mfano katika Dodoma ,Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) lakini sasa watazipata huduma kwenye maeneo wanayoishi," amesema.


Masunga alisema madaktari bingwa hao watakapokuwa wanatoa huduma hizo watawajengea uwezo watumishi wa afya waliopo kwenye vituo vya kutolea huduma ambapo watanufaika na ujuzi na maarifa.


"Tunaendelea kumshukru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha mpango huu kama mnavyofahamu vituo vingi vimejengwa na miundombinu ni wezeshi hivyo tutaendelea kuongeza nguvu kazi kusudi wananchi waendelee kunufaika na huduma za matibabu zilizo bora," amesema.


Masunga alisema utaratibu huu wa kupeleka madaktari bingwa kwenye vituo vya kutolea huduma ambao utakuwa endelevu utapunguza adha za rufaa na kuwapunguzia wananchi mzigo wa kwenda kutafuta huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali.


Naye Katibu Tawala Mkoa  wa Singida,Dk.Fatuma Mganga, amempongeza rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hii kwani itawapunguzia wananchi kwenda kufuata huduma za matibabu ya kibingwa mwenye hospitali nyingine.


Alisema  hospitali zote zilizopo mkoani Singida zina vifaa vyote vya matibabu vya kutosha na kuwahakikishia madaktari bingwa kuwa watapata ushirikiano mkubwa kutoka serikali ya mkoa ili azma ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi iweze kufanikiwa na mkoa kushika nafasi ya kwanza.


Dk.Mganga aliwataka madaktari bingwa hao kuhakikisha wanatoa huduma vizuri kwa wananchi na kutozua sintofahamu zozote ambazo zinaweza kusababisha malalamiko ya wananchi.


"Sitegemei kuona daktari ameleta sintofahamu kutoka pengine amekunywa pombe,sitegemei kuona malalamiko kutoka kwa wateja watakaofika kufuata huduma,tuzingatie kanuni n maadili ya kazi zetu,"amesema.


Aidha, Dk.Mganga alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk.Victorina Ludovick kuweka wauguzi kwenye hospitali ambazo madaktari bingwa watatoa huduma ambao watasaidia madaktari hao kufanya kazi kwa urahisi na haraka.


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Ludovick aliishukru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hii ambayo ni msaada mkubwa kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI