Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wananchi wa Kijiji cha Pamila Halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma wamemkataa Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kijiji hicho Abdallah Mkwiche aliyesababisha Mama mjamzito kujifungulia nje ya zahanati huku Mganga huyo akikataa kutoa huduma na kujifungua ndani ya zahanati.
Wananchi hao wametoa kauli hiyo mbele ya mbunge wa jimbo la Kigoma kaskazini, Asa Makanika aliyefika kijijini hapo kutoa misaada mbalimbali ya chakula kwa wahanga na vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao walipata madhara ya nyumba zao kuezuliwa na mvua.
Mmoja wa waathirika wa vitendo vya mganga huyo wa zahanati,Amina Hussein Nyanzala alisema kuwa alifika zahanati hapo baada ya kupata uchungu akikaribia kujifungua lakini Mganga huyo alikataa kumuhudumia na kumtaka aende kituo cha afya Rusesa wilaya ya Kasulu akimwacha mama huyo mjamzito nje ya milango ya zahanati na bahati mbaya mama huyo akajifungua bila msaada wowote.
Mwananchi mwingine wa Kijiji hicho, Sharifu Chiza alisema kuwa ikifika saa moja usiku Mganga huyo anafunga milango na hakuna huduma yeyote inayotolewa hadi asubuhi hivyo wananchi hao wamekuwa na mateso makubwa kupata huduma kwenye zahanati hiyo hivyo inabidi kutumia gharama kubwa Kwenda kituo cha afya Rusesa wilaya ya Kasulu kupata huduma.
Kutokana na malalamiko hayo Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Asa Makanika amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kigoma kuchukua hatua za kiutumishi kwa mganga huyo ikiwemo kumuhamisha kituo hicho huku akitoa ahadi ya kulipa malipo ya mlinzi kwa mwaka mmoja huku akiitaka halmashauri na uongozi wa serikali ya Kijiji kuweka taratibu za kuwa na mlinzi wa kudumu.








0 Comments