Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Kutokana na changamoto kubwa ya upungufu wa walimu katika shule nyingi nchini Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Mkoani Njombe wameitaka Halmashauri hiyo kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea badala ya kuwaachia wazazi pekee.
Hoja hiyo imeibuka katika mkutano wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo huko Kidegembye ambapo baadhi ya madiwani akiwemo Innocent Gwivaha,Paulo Kinyamagoha na Isaya Myamba wamesema Ifike wakati sasa halmashauri iingilie kati suala la kuwalipa walimu wa kujitolea ili kunusuru elimu ya watoto na sio kuwaachia wananchi.
Makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Njombe Melkizedeck Kabelege amemuelekeza mkurugenzi kufanyia kazi suala hilo kwani shule nyingi zina upungufu mkubwa wa walimu.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Christopher Sanga amekiri kupokea maelekezo hayo na kwamba atakwenda kukaa na wataalamu wake kuona namna ya kwenda kutekeleza agizo hilo ili kiwango cha elimu kiendelee kupanda.
Hata hivyo bwana Sanga ameonya tabia ya Walimu wengi wanaopangiwa kufundisha katika Halmashauri hiyo lakini wanaomba kuhama kwa kile kinachotajwa kuwa ni vijijini.
0 Comments