Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wafanyabiashara mkoani Njombe wamesema licha ya serikali kuendelea kuboresha sekta ya biashara lakini bado baadhi ya maofisa wa serikali wamekuwa kikwazo kikubwa kwao kwani wamekuwa wakiwasumbua hadi wanafikiria kufunga biashara.
Wakizungumza Mbele ya Rais wa Chama cha wafanyabiashara,wakulima na wenye viwanda Tanzania Chamber Of Comerce Taifa [TCCIA]baadhi ya wafanyabiashara hao akiwemo Seth Yohana,RD Sanga,Sophia Mtewele na Onesmo Mwajombe wanasema wamekuwa wakipata adha kubwa katika kituo cha ukaguzi mizigo Mikumi pamoja na mlundikano wa kodi jambo ambalo wanaomba kusaidiwa.
Wamesema usumbufu toka kwa maofisa wa kodi na ushuru umekuwa mkubwa unaosababisha kuwapo kwa mianya ya Rushwa huku wilaya ya Wanging'ombe ikitupiwa lawama ya kutoza ushuru mkubwa wa mazao hususani parachichi.
Ofisa biashara mkoa wa Njombe Lusungu Mbede anakiri kupokea maelekezo na hoja za wafanyabiashara na kwamba ataendelea kuzifanyia kazi zilizopo ndani ya uwezo wake.
Aidha Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Njombe Menard Mlyuka Amesema mashirikiano baina yao na wafanyabiashara ndio yanayowezesha kupata tija katika masuala ya kibiashara.
Kwa upande wake Rais wa TCCIA Taifa Bwana Vicent Minja amesema changamoto hizo ataziwasilisha serikalini ili zikapatiwe ufumbuzi kwani baadhi ya kero ikiwemo mlundikano wa kodi kwenye bidhaa moja zimeshashughulikiwa.
Awali mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe.Antony Mtaka alipokutana na Rais Huyo ofisini kwake amesema yuko tayari kutoa ushirikiano kwa namna yoyote kwani yeye ni muumini wa sekta binafsi ambayo imekuwa ikilisaidia taifa kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na changamoto hizo lakini wafanyabiashara hao wametakiwa kuwa weledi kwa kufanyabiashara halali na si kwa ujanja ujanja.
0 Comments