Bohari za Dawa za nchi za SADC na viongozi mbalimbali wa Sekta ya Afya wamekutana leo Jijini Dar es Salaam kuzindua mfumo wa taarifa za dawa na vifaa tiba ambazo zinapatikana katika nchi za SADC kupitia mfumo huo ambapo utarahisisha katika upatikanaji wa huduma hizo muhimu.
Aidha, hatua hiyo ni muhimu katika kuelekea makubaliano ambayo wamewekeana viongozi hao, kuwa na manunuzi ya pamoja ya bidhaa za afya kwani wanapoenda kununua kwa pamoja nje ya ukanda wa SADC inaongeza nguvu zaidi na gharama kuwa nafuu na kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema kupitia mfumo huo utaweza kujua na kupata taarifa za dawa, bidhaa na vifaa tiba na sehemu vinavyopatikana pamoja na muda kuisha matumizi.
"Mfumo huu ni nyenzo muhimu katika sekta ya Afya wa kuhamasisha ushirikiano miongoni mwa nchi za SADC katika afya za watu wetu hivyo madawa na vifaa tiba ni muhimu katika kulinda Afya ya Binadamu “Amesema Dkt. Jingu.
Hata hivyo, amesema kwenye kanzi data hiyo itaonyesha bidhaa za sekta ya afya zinapatikana wapi na gharama yake na kwa urahisi kuwafikia wahitaji.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Mfumo huo Calicious Tutalfe amesema SADC kupitia mfumo huo wataweza kubadilishana taarifa muhimu hususani za manunuzi pamoja na kufanya maamuzi ya bidhaa gani wanunue.
Aidha, amesema watatumia mfumo huo kupata bidhaa bora na nafuu kupitia taarifa watakazozipata kwenye mfumo na kutengeneza mpango ambao watausimamia.
Naye, Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa Tanzania, Tukai Mavere amesema kuwa, wamefanya mapitio pamoja na viongozi wenzao wa Sekretarieti ya SADC ambapo wameangalia vitu vikubwa vitano ikiwemo kubadilisha namna ambavyo wanatekeleza manunuzi ya pamoja, na kuunda chombo kimoja cha biashara kitakachowaunganisha.
Aidha, ameongeza, kanzi data hiyo waliozindua itatumika kutunza taarifa za bidhaa za afya za nchi za SADC ambapo kila nchi itakuwa na taarifa zake.
Amesema kuwa, taarifa hizo zitahusu bidhaa inayohusika na nchi inakotoka ambapo itasaidia watu kujua nchi tofauti zinapataje bidhaa zake na bei.
Hata hivyo, amesema jukumu kubwa la MSD leo ni kuwasilisha njia ambazo wanazozitumia ili kuhakikisha mfumo huo unakuwa vizuri kwani walipoanza kuna vitu vingi havikuwa sawa kwenye utekelezaji wake.
"Hata mfumo wake wa utekelezaji ambao ulikuwa unaenda kutumika, haukuweka mazingatio makubwa kwenye maeneo muhimu kama sheri za manunuzi, fedha, masuala ya udhibiti ubora, usajili wa bidhaa katika nchi husika pamoja na namna ya mfumo kufanyia kazi malipo kati ya mnunuzi na muuzaji".
0 Comments