NA WILLIUM PAUL, SAME.
KATIBU Tawala mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Same, Jimson Mhagama kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Misufini goma iliyopo kata ya Ndungu.
Nzunda alitoa kauli hiyo mara baada kutembelea shuleni hapo na kujionea ujenzi wake ambapo serikali ilitoa milioni 584.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane, jengo la utawala, jengo la maktaba, maabara tatu, matundu kumi ya vyoo, kichomea taka na miundombinu ya maji.
Alisema kuwa, lengo la serikali kujenga shule hiyo ni kuhakikisha inaondoa adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu na kumtaka Mkurugenzi kuhakikisha shule hiyo inakamilika ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Alisema kuwa, mkoa hauhitaji miradi viporo kabla ya Juni 30 mwaka huu na kumtaka Mkurugenzi kuhakikisha miradi yote inakamilika kabla ya muda huo.
“Mkakati wa mkoa ni kumaliza miradi viporo lakini katika shule hii sijaridhishwa na milango na madawati hivyo nikutake Mkurugenzi muagize fundi aliyetengeneza vitu hivi arudi kufanya marekebisho” alisema Nzunda.
Aidha Katibu Tawala huyo amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri kuweka katika bajeti fedha za uchimbaji wa kisima cha maji katika shule hiyo pamoja na kuanzisha ujenzi wa nyumba za walimu.
Awali akisoma taarifa za ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa shule Adam Mbele alisema kuwa, miundombinu iliyokamilika na kuanza kutumika ni madarasa nane, jengo la utawala na matundu 10 ya vyoo huku jengo la maktaba , Tehama na maabara yapo kwenye hatua ya umaliziaji.
Mbele alisema kuwa, mradi huo umesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya sekondari ya Ndungu pamoja na kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali wa kilomita 7 mpaka 10 kwenda shuleni.
Mwisho…










0 Comments