Na Jusline Marco:Arusha
Takribani hekari 250 za mazao ya mahindi katika Halmashauri ya Meru, wilayani Arumeru ziko hatarini kuharibika kwa kushambuliwa na wanyama aina ya Panya wa mashambani katika msimu huu.
Afisa Kilimo Halmashauri ya Meru Ridhiwani Kombo ameyasrma hayo katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo amesema mlipuko huo wa panya umejitokeza mwaka huu katika baadhi ya Kata ndani ya halmashauri hiyo.
Akibainisha Kata hizo Afisa huyo amesema Kaza zilizokumbwa na janga hilo ni Kata ya Malula,Kikatiti,King'ori,Majengo,Makiba,Shambari Burka na Kikwe ambapo panya hao wamekuwa wakishambulia zao la mahindi ambayo yameanza kukomaa na yaliyoanza kubeba.
Ameongeza kuwa tayari Halmashauri ya Meru imeanza kuchukuwa hatua za kutoa taarifa kwenye taasisi husika ya Afya ya mimea na viuatilifu Tanzania TPHPA pamoja na Ofisi ambayo inashughulika na kudhibiti panya waharibifu iliyopo Mkoani Morogoro ambayo ndiyo inatoa sumu ya kudhibiti panya hao waharibifu na tayari imeahidi kutoa wataalamu wao ili kuweza kufika kwa ajili ya kudhibiti na kuangamiza panya hao kusudi wasiweze kuharibu mazao ya wananchi.
"Tumeshawapa taarifa maafisa kilimo wetu kwa ajili ya matayarisho na tunategemea ndani ya siku mbili hizi watafika kwaajili ya kuanza zoezi hilo na kinachohitajika ni wananchi tu kuchangia chabo ambayo itatumika kuvutia panya hao ambazo ni mahindi,dagaa na mafuta ya kupikia ili tatizo hilo kuanza kushughulikiwa."Alisema Afisa Kilimo huyo.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa wananchi wameshauriwa kutumia sumu ya kuua panya ambayo inauzwa madukani na sokoni pamoja na mitego ya kienyeji ambayo wananchi wanatega ili kuweza kudhibiti panya hao wakati wakiwasubiria wataalam hao kuweza kufika.
Awali Diwani wa Kata ya Majengo wakati akiwasilisha taarifa ya Kata hìyo ameeleza changamoto ambayo imezimba baadhi ya kata ikiwemo Kata ya majengo ambapo ameomba elimu iweze kutolewa kwa wakulima juu ya uchanganyaji wa sumu ya kuwaangamiza panya hao ambao wamekuwa tishio kwao badala ya kusubiri wataalam kutoka SUA Morogoro kuja wachanganya dawa wenyewe na kuwapatia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mwalimu Zainabu Makwinya katika mkutano huo akitoa ufafanuzi wa hoja za madiwani zilizotolewa katika baraza hilo ikiwemo hoja ya mafuriko kwenye baadhi ya Kata,Mwl.Makwinya amewaagiza maafisa Mazingira wa halmashauri,Afisa kilimo na wataalam wake pamoja na DMO kuweza kutembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazonyesha kwa ajili ya kudhibiti athari kwa wananchi zisiendelee kuleta madhara.
Akitolea ufafanuzi hoja katika Sekta ya Elimu Mwl.Makwinya amewataka waheshimiwa madiwani kuelewa kuwa shule zilizopo katika maeneo yao siyo shule za Mkurugenzi wa Halmashauri bali ni shule za wananchi hivyo ni jikumu la watendaji wa Kata na Madiwani wao kushirikiana na halmashauri kufanya maboresho yaliyopo katika shule hizo.
Vilevile Mkurugenzi Makwinya ameeleza kuwa changamoto zilizopo katika Kata haziwezi kutatuliwa na kumalizika kwa siku moja ambapo amewataka pia Madiwani hao kutoa kipaumbele kwenye mambo ambayo niya msingi zaidi ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi na kuelekeza kila Kata na Shule kuweka mpango wa maendeleo kusudi kuweza kutoa urahisi pindi wadau wa maendeleo wanapojitokeza kuunga mkono juhudi za serikali za uletaji wa maendeleo kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Diwani wa Kata ya Imbaseni Jeremia Kishili katika baraza hilo amewaagiza watendaji kuleta taarifa za lishe katika vikao vya baraza la madiwani ili kuweza kupata hali ya lishe kwenye jamii ikoje na kuwataka wataalam wa kilimo kutembelea Kata ambazo hazina maafisa kilimo ili kupunguza adha ya wataalamu wa kilimo na mifugo kwenye maeneo ambayo hayafikiwi na wataalam hao.
Amebainisha kuwa, kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Halmashauri ya Meru kusonga mbele kiafya,kielimu na kiuchumi.
0 Comments