Header Ads Widget

MBUNGE ABOOD AJITOLEA KUKARABATI BARABARA JIMBONI FEDHA ZAKE



Na. Ashton Balaigwa,MOROGORO

KUFUATIA kumalizika kwa Mvua za Masika huku zikiacha maumivu kwa wananchi kutokana kuharibika kwa makazi na Miundombinu ikiwemo ya Barabara,Mbunge wa Jimbo la Morogoro(CCM) AbdulAziz Abood amemua kurejesha kwenye hali yake miundombinu ya Barabara kwa kutumia fedha zake binafsi.


Hatua ya Abood kuamua kukarabati miundombinu hiyo ya barabara  inatokana na siku za hivi karibuni Gari la Zimamoto kushindwa kwenda kutoa huduma kutokana na barabara kutopitika baada ya moja ya Nyumba kuungua katika kata Lukobe na kusababisha vifo vya watoto wawili.

Mbunge Abood kwa kutumia mitambo yake ya kutengeneza miundombinu ameanza kuzifanyia ukarabati barabara za mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro ambazo kwa muda mrefu sasa hazipitiki kutokana na kuharibika.

Akizungumza wakati akikagua maendelea ya ukarabati huo katika barabara za mitaa mbalimbali,Abood alisema ameamua kufanya ukarabati huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kurejesha kwenye hali yake ya kawaida ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

“ Wakati wa Kampeni zangu kila nilipopita nilihaidi kusaidia ujenzi wa miundombinu mbalimbali,sasa wote tumeona Mvua zilizonyesha zimeharibu kabisa barabara zetu katika kata mbalimbali na hazipitiki kama Mbunge wao siwezi kukaa kimya lazima niwasaidie zipitike ndio maana nafanya hivyo” alisema Abood.

Abood alizitaja Barabara zilizoanza kukarabatiwa ni kutoka katika Kata za Kiwanja cha Ndege,Mafisa,Chamwino,Lukobe,Kihonda na Kihonda Maghorofani ambazo mpaka sasa tayari zimeshaghalimu jumla ya sh milioni 45.

“ Mimi ni Mbunge wa vitendo sio wa maneno maneno ya jukwaani wakati wananchi wanapata shida,nimeona kuna changamoto barababara hazipitiki nimeamua kugharamia kwa fedha zangu kurejesha miundombinu hii ni kuunga mkono juhudi za Mama yetu na Rais wetu Samia Suluhu Hassani” alisema Mbunge huyo.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Lukobe,Siasa Abdallah balozi wa mtaa wa lukobe ,alimshukuru Mbunge huyo kwa kazi ya kukarabati barabara za kata ya Lukobe na maeneo mengine kwani imesaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Naye Katibu wa CCM wilaya ya Morogoro mjini,Twalib Berege,alisema  mvua zilizomalizika zimeacha  uharibifu mkubwa wa miundombinu hususani barabara na kutokana na  bajeti ya Serikali ukarabati ungechelewa lakini Abood ameamua kuzitengeneza hizo barabara ili kurudisha mawasiliano na huduma kwa wananchi.

Meya wa Manispaa ya Morogoro,Paschal Kihanga,alisema kitendo kinachofanywa cha Mbunge Abood ni uzalendo kwa wananchi wake pamoja na Taifa kwa ujumla kwani amekuwa ni mtu wa kutatua kero kwa wakati  zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo la Morogoro mjini.

Mwisho.

MAELEZO YA PICHA

Baadhi ya Mitambo ya kutengenezea Barabara ya Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini,AbdulAziz Abood,ikifanya ukarabati kwenye Barabara ya Mtaa wa Lukobe Manispaa ya Morogoro iliyoharibika kutokana na Mvua za Masika,Picha Nyingine Barabara ya Lukobe baada ya kufanyiwa ukarabati na Mbunge wa Jimbo hilo la Morogoro mjini AbdulAzizi Abood aliyejitolea kukarabati barababara kwenye kata zote za Manispaa ya Morogoro.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI