Dk Bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Mwanaada Kilima.
NA MWANDISHI WETU
Matumizi ya tumbaku katika umri mdogo husababisha athari za mapema za kuzorota kwa afya ya akili, mapafu, ukuaji na mwili mzima kuathirika kwa kiasi kikubwa hivyo kuchangia upotevu wa nguvu kazi katika taifa.
Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mwanaada Kilima akielezea Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku ambayo huadhimishwa Mei 31 kila mwaka ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa watu wote kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku, kuongeza msukumo kwa watunga Sera na mamlaka mbalimbali ili kuendeleza zuio la matumizi ya tumbaku.
Amesema, kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani, watoto ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya tumbaku na sigara.
“Matumizi ya sigara yapo katika mfumo ambao unawarubuni watoto na vijana ambapo bidhaa hizo zipo katika namna ya ushawishi na mifumo mbalimbali ya kielektroniki kama bomba au saa” amefafanua Dk. Kilima.
Dk Kilima ameongeza kuwa matumizi ya tumbaku na sigara husababisha vifo na mdhara makubwa ya afya hivyo huchangia magonjwa yasiyoambukizwa ambapo asilimia 90 ya uvutaji wa sigara husababisha saratani mbalimbali ikiwemo ya mapafu, shingo na kichwa, tumbo, shinikizo la juu la damu, kiharusi, mshtuko wa moyo, maradhi ya akili n.k
"Natoa wito kwa vijana, watoto na watu wote kuacha matumizi ya tumbaku na aina zozote za sigara ikiwemo sigara za kielektroniki na nyinginezo maarufu kama (shisha) kwani matumizi yake kwa saa shisha moja ni sawa na kuvuta sigara mia moja na huleta madhara makubwa." amesema
Kauli mbiu ya Siku ya kutotumia tumbaku mwaka huu ni “Tuwalinde watoto dhidi ya urubuni wa makampuni ya tumbaku”.
0 Comments