Header Ads Widget

MASIKINI MSIGWA NDIO BASI TENA UENYEKITI CHADEMA KANDA YA NYASA,SUGU AMSHINDA KWA KURA MBILI

 

TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII


SUGU AMBWAGA MSIGWA UENYEKITI KANDA, ASEMA HAJASHINDA BALI CHADEMA NDIO IMESHINDA.

NA JOSEA SINKALA, MAKAMBAKO NJOMBE.

Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Osmund Mbilinyi (Sugu), ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Nyasa baada ya kumshinda mpinzani wake Mchungaji Peter Msigwa na kuahidi utumishi shirikishi katika kuongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Sugu ambaye pia amewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA Taifa, ameshinda katika jumla ya kura 106 ambapo amepata kura 54 sawa na asilimia 51 wakati Mchungaji Peter Msigwa akipata kura 52 sawa na asilimia 49.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa Baraza la uongozi Kanda ya Nyasa uliofanyika mjini Makambako Mkoani Njombe, Msimamizi wa Uchaguzi huo Naibu katibu mkuu wa CHADEMA (Bara) Benson Singo Kigaila, amemtangaza Joseph Mbilinyi (Sugu) kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2024 - 2029).

Akizungumza baada ya kuibuka mshindi kwenye nafasi hiyo, Sugu ameahidi utumishi mwema na uadilifu kwa maslahi ya chama na wananchi kwa ujumla akihitaji zaidi ushirikiano kwa viongozi wa nafasi zote za juu na chini yake ili kutimiza shauku yake kuendeleza kazi ya kukijenga chama hicho kuanzia alipoishia mtangulizi wake Mchungaji Peter Msigwa.

Sugu amesema katika vipaumbele vyake kumi ni lazima ushirikiano miongoni mwao uwepo na kuhakikisha kwenye chaguzi zijazo kuanzia Serikali za mitaa wanashinda.

"Nataka niwaambie huu uchaguzi Chama (CHADEMA) kimeshinda na sio Sugu ameshinda. Kazi tuliyo nayo ni kwenda kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani (2025), mimi peke yangu siwezi kutimiza vile vipaumbele vyangu nilivyokuwa nanadi kwenye ilani wakati wa kampeni", amesema Sugu na kuongeza.

"Tukitoka hapa (Makambako Njombe) kuanzia terehe 29.05.2024 tukawe kitu kimoja na mimi kazi yangu ya kwanza ni kwenda kuwaunganisha wanachama ili kuishinda CCM na sio kupingana sisi wenyewe kwahiyo twendeni tukashikamane kuanzia kesho Mei 30, 2024 tukaanze kazi moja kuhakikisha tunashinda Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao ", ameeleza Mwenyekiti huyo mpya wa CHADEMA Kanda ya Nyasa.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wagombea wote ambao kura hazikutosha, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Mchungaji Peter Simon Msigwa amempongeza Joseph Mbilinyi kwa ushindi huo akisema ndio Demokrasia na nafasi hizo ni za kubadilishana.

"Nawashukuru sana viongozi wote wa mkutano huu, kura ndio zimeamua hivyo mmepata mlichokitaka na nikupongeze Sugu kwa kupata nafasi hiyo, mimi sikuja kwenye chama hiki ili kutaka cheo nitaendelea kuwa mwanachama yeyote anayehitaji ushauri na chochote tuambiane tuzidi kushirikiana, sihitaji cheo ili kuwa bora, nawashukuru sana ", amesema Msigwa ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Iringa mjini.

Sanjari na hayo katika nafasi ya makamu mwenyekiti wa Kanda, Kigaila amemtangaza Frank George Mwakajoka ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya wagombea Kanda ya Nyasa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduma Mkoani Songwe aliyewashinda wenzake wawili akiwemo aliyekuwa kwenye nafasi hiyo Joseph Mwasote (China).

Hata hivyo katika nafasi ya mweka hazina wa CHADEMA Kanda ya Nyasa ameibuka mshindi Bi.Grace Shio kutoka Mkoani Rukwa akiwashinda wenzake wawili.

Kwenye nafasi za mabaraza, Baraza la wazee wa CHADEMA (BAZECHA) ameshinda Charles Dawson Ndenga, Baraza la wanawake BAWACHA ameshinda Tabia Kilasi Mwakikuti na nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa CHADEMA BAVICHA Kanda akiibuka mshindi Vitus Nkuna kutoka Mkoani Iringa.

Wakizungumza baada ya matokeo hayo, baadhi ya viongozi wa CHADEMA wamesema ni imani yao kuwa umoja na mshkamano utadumishwa ndani ya chama hicho ili kuhakikisha wanaunganisha nguvu na kwenda kupambana na kuibua washindi kwenye chaguzi zijazo za kiserikali bila kuruhusu makundi ndani ya chama chao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI