Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego
MKURUGENZI wa Chuo cha Mtakatifu Gaspar,PADRE JUSTIN BONIFACE
Na Thobias Mwanakatwe, ITIGI
HOSPITALI YA Mtakatifu Gaspar inayomilikiwa na Kanisa Katoliki iliyopo Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida imeadhimisha miaka 35 ya huduma hukh Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akiipongeza kwa uwekezaji mzuri wa vifaa na mazingira safi ya hospitali hiyo yanayovutia.
Akizungumza jana wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya huduma ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Dendego alisema katika kukagua hospitali hiyo amefurahishwa na jinsi uwekezaji mkubwa wa vifaa ulivyofanyika na kikubwa zaidi ni jinsi mazingira ya hospitali hiyo yalivyo mazuri na yanavyovutia.
Alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya Mtakatifu Gaspar ili iendelee kutoa huduma bora zaidi na kwamba ndoto kubwa aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan ni kupambana na vifo vya akina mama na watoto.
Dendego alisema serikali imejenga vituo vingi vya afya na zahanati ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kwamba katika kufanikisha utoaji wa huduma za afya ni lazima kushirikiana na taasisi binafsi.
"Tunawashukuru,tunawaheshimu na kuwathamini sana wamisionari wanaotuunga mkono, nikuombe Mkurugenzi kama kuna changamoto zozote mnazozikabili nikabidhini nizitafutie ufumbuzi na nimefurahishwa jila nilipopita kukagua nimekuta wanaohudumia ni vijana," alisema Dendego
Aidha,Mkoa wa Singida aliwataka vijana kujitambua na kufanya kazi kwa bidii ambayo jamii inaiona kwa macho badala ya kupiga kelele kwenye mitandao ya kijamii.
"Niwaombe vijana wa Itigi,Manyoni,Singida na Tanzania kwa ujumla wafike hapa St Gaspar waone jinsi wenzao wanavyochapa kazi vijana sio kelele kwenye mitandao vijani ni kujitambua na kufanyakazi ambayo jamii inaiona kwa macho," alisema .
Naye Mkurugenzi wa Hospitali na Chuo cha Mtakatifu Gaspar, Padre Justin Boniface, alisema taasisi Mtakatifu Gaspar imepata mafanikio sana tangu kuanzishwa kwake 1987 kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini.
Alisema katika maadhimisho haya mwaka huu taasisi imeboresha huduma zaidi kwa kukarabati wodi ya wanawake na kuwekewa vifa vifya vya kisasa ili kuwawezesha akina mama kupata huduma bora.
Padre Boniface alisema mwaka huu pia hospitali imeanza kujenga kitengo cha kusafisha damu ambacho kwa Mkoa wa Singida huduma hiyo inatolewa sehemu moja tu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota, aliwapongeza wafanyakazi kwa kazi nzuri wanazofanya na kuwataka waendelee kuifanya kwa bidii ili sifa zilizopo katika taasisi hiyo zifike zaidi kimataifa.
Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar ilianza kama zahanati 1987 na mwaka 1989 ilizinduliwa rasmi kwa ngazi ya wilaya na Rais Ali Hassan Mwinyi.
0 Comments