Header Ads Widget

DK.CHUWA : WANAWAKE CHUKUENI FOMU KUWANIA UONGOZI TUFIKIE SERA YA 50 KWA 50

 

Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Dk. Albina Chuwa akizungumza wakati wa semina kwa viongozi wilayani Iramba

Na Thobias Mwanakatwe,IRAMBA

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchauzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu  2025 ili kuweza kufikia sera ya 50 kwa 50.

Alisema hayo jana (Aprili 6, 2024)  wakati wa semina kwa viongozi kuhusu mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kizaga wilayani Iramba mkoani Singida.

Dk.Chuma alisema kutokana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2022 zinaonesha wanawake ni wengi nchini hivyo ni vyema wakatumia uwingi huo kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Dk Albina alisema takwimu zinaonesha kuwa katika Wilaya ya Iramba wanawake wanaongoza  kwa sababu wapo 165, 000 huku wanaume wakiwa 163,000.

"Wanawake wenzangu tunakazi, tumesoma, tuna sera ya 50 kwa 50, hivyo tukachukue fomu kuwania uongozi kwa sababu takwimu zimekwishatuonesha tupo wengi," alisema Dk.Chuwa

Dk.Chuwa alisema kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 inaonyesha kuwa kiwango cha watu kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea wanaojua kusoma na kuandika kimeongezeka hadi asilimia 83.

Alisema kuwa wamepiga hatua kufikia kiwango hicho ukilinganisha na asilimia takribani 44 kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida una asilimia 70 huku kwa Wilaya ya Iramba wakiwa asilima 68  ya watu wanaojua kusoma na kuandika kwa lugha yoyote.

Dk.Chuwa alisema hatua hiyo ni kubwa hivyo kuwataka viongozi kuungana na serikali yao kwa kwenda kuzifanyia kazi takwimu hizo kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alisema wilaya hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo ambapo wakati anateuliwa kuiongoza Iramba, alikuta vijiji 54 ndio vyenye umeme huku hivi sasa vijiji vyote 70 vya wilaya hiyo vinaumeme.

Alisema kuwa vitongoji 189 vinanishati hiyo huku akiweka wazi kuwa wananchi hao wanapata ruzuku toka serikalini pindi wanapolima.

"Furaha ya mara mbili  wanayoionesha wananchi wangu imeletwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anabebwa na takwimu zinazoeleza mambo mbalimbali aliyoyafanya nchini," alisema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), anayewakilisha wanawake wa Mkoa wa Singida, Grace Mkoma amemshukuru Dk. Chuwa  kwa kutoa elimu itokanayo na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mkoma amewataka viongozi walionufaika ma mafunzo hayo  kwenda kuyafanyia kazi yote waliofundishwa ikiwemo kuifikishia jamii inayowazunguka.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS