Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAVUVI wanaofanya shughuli zao kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wamepatiwa boti tisa za uvuvi ikiwa kuunga mkono juhudi zao katika kuimarisha shughuli hizo za uvuvi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mitumbwi hiyo Msimamizi wa miradi ya Taasisi ya African Relief Organization kwa mkoa Kigoma, Gwanko Mahamudu Kamana alisema kuwa kukabidhiwa kwa mitumbwi hiyo kunatimiza idadi ya mitumbwi 24 yenye thamani ya shilingi milioni 60 ambayo taasisi hiyo imekabidhi kwa wavuvi wa mwambao wa ziwa Tanganyika mjini Kigoma.
Msimamizi huyo wa miradi ya African Relief Organization mkoa Kigoma alisema kuwa mitumbwi hiyo imekabidhiwa ikilenga kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Kigoma kupitia shughuli za uvuvi.
Kwa upande wake Akizungumza katika makabidhiano hayo Shekhe wa mkoa Kigoma,Hassan Iddi Kiburwa amewataka wavuvi waliokabidhiwa mitumbwi hiyo kuifanyia kazi na kuleta matokeo kama ilivyokusudiwa ili kuwatia moyo wafadhili hao waweze kusaidia watu wengine Zaidi.
Awali Mwenyekiti wa wavuvi mkoa Kigoma, Mohamed Kasambwe alisema kuwa mitumbwi hiyo itaongeza idadi kubwa ya ajira kwa watu wanaofanya shughuli za uvuvi kutokana na mtumbwi mmoja kuwa na wafanyakazi 15.
Pamoja na hilo Kasambwe ameomba wavuvi kupatiwa elimu ya uokoaji kwani inapotokea Dhoruba ndani ya ziwa kwa boti au meli kupata majanga ya kuzama wao ndiyo wanakuwa karibu kwa sababu muda mwingi wapo ndani ya ziwa hivyo misaada ya vifaa hivyo iende sambamba na elimu mbalimbali ikiwemo elimu ya ufugaji Samaki kwenye vizimba.
0 Comments