Header Ads Widget

WASICHANA WENYE UMRI KATI YA MIAKA 9 HADI 14 KUPEWA CHANJO YA SARATANI SINGIDA


Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

WASICHANA 178,114 wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 katika Mkoa wa Singida wanatarajia kupatiwa chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi (HPV) ili waweze kujikinga na maambukizi ya virusi vinavyosababishwa na ugonjwa huo.


wanafunzi wa kike wakipata chanjo picha ya mtandao 

Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginoma, amesema hayo leo wakati wa  kikao cha uhabarisho ngazi ya mkoa kilichowajumuisha wakuu wa wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri, viongozi wa dini,kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wataalamu wa afya kutoka wilaya zote za Mkoa wa Singida.


Amesema chanjo hiyo itaanza kutolewa Aprili 22 hadi 26, 2024 kwa wasichana wote wenye umri wa miaka 9nhadi 14 waliozaliwa kati ya mwaka 2010 -2015  na kwamba katika kuhakikisha chanjo inafanikiwa mkoa umepokea chanjo za kutosha dozi 191,940 na usambazaji kwenda ngazi ya halmashauri unaendelea.


Mhanginoma amesema hali ya uchanjaji kwa Mkoa wa Singida katika kipindi cha kuanzia 2018 hadi 2024 waliopata dozi ya kwanza walikuwa 131,677, dozi ya pili 96,932 na ambao hawakukamilisha dozi ya pili walikuwa 34,745.


"Chanjo ya saratani ya mlango wa uzazi nchini Tanzania iliidhinishwa na Shirika la Afya Dunia (WHO) na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa  na Vifaa Tiba (TMDA) mwaka 2014 ambapo ilianza kutolewa katika mkoa wa Kilimanjaro na mwaka 2018 ilianza kutolewa nchi nzima," amesema.

Mhanginoma amesema chanjo hiyo inatolewa kwa wasichana kutokana na sababu za kibailojia na kiuchumi ambapo wanawake huathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi hivyo kuwakinga kutapunguza maambukizi kwa wanaume kwasababu ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia za kujamiana.

Naye Mkuu  wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliwataka viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini kuwaelimisha wazazi wenye watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 kuwapeleka kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi itakayoanza kutolewa mkoani hapa April 22, 2024.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mwana Dk.Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kuhakikisha wanawake wanapewa chanjo hiyo lengo kuwafanya wanapofikia umri wa kuwa 'active' katika masuala ya kujamiana wawe na kinga hasa kutokana ugonjwa huu unaambukiza kirahisi kwa njia ya kujamiana.


"Tumeitana kama wajumbe wa kamati na kama viongozi kwneye jamii tunajua jamii zetu zina mitazamo tofauti na tunaishi kwenye mila na desturi tofauti lakini hili lazima tuungane sote kwasababu madhara ya ugonjwa huu yanatuathiri sisi wote bila kuangalia tofauti ambazo tunazo," amesema.

Dendego amesema ili kuweza kufanikisha chanjo hii viongozi wote ambao wana ushawishi mkubwa kwenye jamii wasaidie kuwahamisha wazazi ambao wana wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 kuhakikisha wanapata chanjo ya saratani ya mlango wa uzazi.


"Chanjo hii inatolewa bure, sote tunatambua mwanamke ndo mlezi wa familia na mwanamke pia ana mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi,kwa hiyo muda wote tunataka wamama wawe salama ili watimize jukumu lao la kibailojia walilopewa na mwenyezi Mungu lakini pia watimize majukuya kijamii na kiuchumi," amesema.

Dendego amesema kwa kuwa chanjo hiyo ilianza kutolewa 2018 wale ambao wakipata chanjo kipindi hicho wawe wanashirikishwa kwenye zoezi la kuhamasisha wengine ili wajitokeza wanawake wengi kupata chanjo.


Nao washiriki wa kikao hicho waliiombe serikali kutoa vipeperusha vitakavyoelezea chanjo hiyo na umuhimu wake ili watakapokuwa wanawaelimisha wananchi iwe rahisi kuelewa.






MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS