Na Thobias Mwanakatwe,IRAMBA
WALIMU na wanafunzi katika shule za msingi wilayani Iramba mkoani Singida wamepewa motisha ya zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu Sh.milioni 14.5 kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya taifa ya darasa la nne na saba iliyofanyika 2023.
Motisha hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, kwa walimu na wanafunzi 10 waliofaulu kwa kiwango cha juu kwenye mitihani hiyo.
Katika hafla hiyo, walimu waliofaulisha vizuri katika masomo yao, shule zilizoongeza ufaulu na shule zilizoongoza kwa kata zilipewa zawadi ya kompyuta.
Zawadi nyingine zilitolewa kwa shule bora sita zilizoongoza kiwilaya kwa ufaulu, kata zilizoongeza ufaulu kiwilaya, shule binafsi zilizoongoza ufaulu kiwilaya na shule iliyoongeza ufaulu kwa kiasi kikubwa sana kiwilaya
Mwenda akizungumza na walimu hao alisema kazi ya ualimu ni wito ambao ukiitwa unatakiwa kuitika kwa kuifanya vizuri ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule yako.
"Najua uwezo wenu ndo maana pale ambapo panahitajika kuongeza nguvu tunachukua hatua na mimi kama kiongozi wenu naridhika na mabadiliko ambayo mnayaonyesha katika maendeleo ya elimu na kuongeza ufaulu," alisema.
Alisema alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya Iramba alikuta kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 58 lakini jitihada kubwa zimefanyika ambapo ndani ya miaka 3 kiwango kimeongezeka na kufikia asilimia 71.9.
"Lengo letu ilikuwa ni kufikia asilimia 85 lakini kwa sasa Mkuu wa Mkoa Singida, Halima Dendego amekuja na lengo lake, na kwa kuwa Mkuu wa Mkoa ni kiongozi wetu wa mkoa yeye amelenga kufikia asilimia 90 hivyo naamini kwa msimu huu tutajitahidi tufikie lengo hilo," "alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora alisema haki ya mwalimu inatakiwa itolewe kwake lakini na mwalimu naye anapaswa kutekeleza wajibu wake.
"Walimu wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao matokeo huwa yanajionyesha kwenye matokeo ya mitihani ya taifa inayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)," alisema.
Mwenyekiti wa Huduma za Jamii, Wilfred Kizanga, aliwataka walimu kishirikiana na kuondoka katika nafasi za mwisho kwani Iramba siyo mrithi wa nafasi hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi, aliwataka Maafisa Elimu Kata kuvua vyeo vyao na kushirikiana na walimu ili kuhakikisha wilaya inashika nafasi ya kwanza kimkoa.
0 Comments