Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi Justine Masejo amesema wameanza kutekeleza kikamilifu maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Makonda katika kuhakikisha Ulinzi na usalama unaimarika mkoani humo.
Kamanda ACP Masejo ametoa kauli hiyo kufuatia maelekezo ya Mkuu wa mkoa wa Arusha kutaka usalama kuimarishwa ili kuwezesha biashara na shughuli nyingine za utalii kufanyika kwa saa 24.
Pia, amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kufunga kamera na taa kwenye maeneo yaliyokuwa na wingi wa matukio ya kiuhalifu ili kusaidia kubaini uhalifu na wahalifu wa katikati ya Jiji.
Amesema lengo ni kuhakikisha mkoa mzima unakuwa na Kamera katika maeneo yote ili kusaidia katika doria na ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Aidha Kamanda Masejo, amehimiza suala la Maadili kwenye ngazi za familia na kuwalea vijana vyema katika hofu ya Mungu ili kusaidia katika kupunguza matukio ya kiuhalifu kwenye jamii.
Katika hatua nyingine, Kamanda Masejo ameongelea kundi la vijana linalojiita Wadudu waliopo mkoani Arusha na kusema kuwa vijana hao siyo wahalifu kama ambavyo jamii inavyowatazama bali ni wasanii ambao wanafikisha ujumbe kwa njia tofauti kwa kutmia mavazi yao.
Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Paul Makonda amekuwa akisisitiza mara kadhaa kuhusu usalama ndani ya mkoa wa Arusha kama sehemu ya kuendelea kukuza na kustawisha utalii na biashara ndani ya mkoa wa Arusha ulio kitovu cha utalii na Diplomasia kwa ukanda huu kutokana na vivutio vya utalii vinavyopatikana mkoani Arusha pamoja na ofisi mbalimbali za Kimataifa na kumbi kubwa za mikutano.
0 Comments