Header Ads Widget

SUGU AKUBALI MDAHALO NA MSIGWA KITI CHA CHADEMA NYASA

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Mbilinyi (Sugu) amesema yuko tayari kukutanishwa na Mchungaji Peter Msigwa kwa ajili ya mdahalo ambapo wote wawili wanagombea nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa.


Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Mbeya mjini ambaye kwa sasa anaomba kugombea uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, amesema hayo kupitia moja ya ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.


Bila kumtaja wazi jina, Sugu amesema ni jambo jema na yuko tayari muda wowote kukutana na mgombea uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Peter Msigwa ikiwa utaandaliwa.


"Nasikia kuna mtu huko anataka mdahalo na mimi... Well (vizuri), niko tayari any time (muda wowote), Asante, 'TAITA' NYASA MPYA", ameandika Joseph Mbilinyi.


Siku moja iliyopita Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa anayeomba kutetea nafasi hiyo Mchungaji Peter Simon Msigwa, aliuomba uongozi wa CHADEMA Taifa (Ofisi ya Katibu mkuu) kuwaandalia mdahalo yeye (Msigwa) na mgombea mwenzake Joseph Mbilinyi na wengine wanaowania nafasi hiyo ili kuhojiwa maswali na viongozi wa mkutano mkuu wa Kanda kwa lengo la kupimwa uwezo wao wa kiuongozi akisema anajiamini bado anatosha na ana nia ya kweli kuendelea kuwatumikia wanachama wa CHADEMA Kanda ya Nyasa na si mtu mwingine yeyote.


“Ninahitaji kuona CHADEMA tunashinda kila kiti kwenye ngazi zote (Uchaguzi wa Serikali za mitaa na vijiji) hadi uchaguzi mkuu (2025). Lakini namuomba Katibu Mkuu (John Mnyika) atupe mdahalo mmoja na Sugu (mgombea uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa) ili tushindanishe sera zetu, tuone nani mwenye uwezo. Chama hiki kinahitaji watu wenye uwezo kukitangaza kama ambavyo tumeisimamisha Mbeya kwa muda", alisema Msigwa na kutoa shukrani zake kuwa


“Ninawashukuru na kuwapongeza kwa mapokezi makubwa na huu ndio ushindi rasmi umeanza, hadi sasa naona kura zangu ni 82 kati ya 103 za wajumbe wote, ambapo uhalisia nimeshashinda hao wengine watafute kazi nyingine, Sugu ni rafiki yangu lakini kwenye hili sijamuelewa”, amesema Mchungaji Peter Msigwa.


Uchaguzi wa Viongozi mbalimbali wa CHADEMA Kanda kadhaa hapa nchini unatarajiwa kuanza Mei 2024 kwa ajili ya Chama hicho kupata viongozi watakaowaongoza wanachama kwa miaka mitano ijayo (2024 - 2029) na zoezi hilo limefungwa jioni ya Aprili 22, 2024 jijini Mbeya kwa watia nia kurejesha fomu za kuomba kuwania nafasi mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI