Header Ads Widget

SIMBA, YANGA KUANDIKA HISTORIA AFRIKA?



Klabu mbili kongwe za soka Simba na Yanga kutoka Afrika Mashariki nchini Tanzania, Ijumaa hii April 5 zinakabiliwa na kibarua kizito cha kuwania kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza, zitakaposhuka dimbani katika ncha mbili tofauti za Afrika; Kaskazini nchini Misri na Kusini nchini Afrika Kusini kuwakabili wenyeji Al Ahly na Mamelodi Sundowns.

Hii inaweza kuwa wikiendi ya kukumbukwa zaidi kwa mashabiki wa soka Afrika Mashariki, wakati vigogo wa soka Afrika, Al Ahly wakitafuta kuendeleza historia yao kwa kulibeba taji lao la 12 la Ligi ya mabingwa Afrika

Simba ya Tanzania inaweza kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi za vilabu Afrika tangu kubaldilishwa kwa mfumo wa mashindano hayo mwaka 1998.

Simba iliwahi kufika nusu fainali ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974 katika mfumo wa awali na kutolewa na Ghazil Al Mahalla ya Misri kwa changamoto ya mikwaju ya pentai baada ya matokeo ya jumla ya goli 1-1

Klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam inashuka kwenye mchezo huu ikiwa nyuma kwa goli 1-0 walilofungwa kwenye mchezo wao wa mkondo wa kwanza nyumbani Machi 29, hivyo wanalazimika kuifunga Al Ahly walau magoli 2-0 au ushindi mwingine wowote wa tofauti ya magoli mawili ili kufuzu moja kwa moja kwa hatua inayofuata. Lakini hata ushindi wa goli 1-0 utawapeleka kwenye changamoto ya mikwaji ya penati.

Mchezo huu wa aina yake unatarajiwa kuvuta hisia za wapenzi wengi wa soka kutokana na matokeo ya hivi karibuni baina ya Simba na Al Ahly.

Mara ya mwisho Ahly kupata ushindi mkubwa mbele ya Simba ilikuwa mwaka 2019 waliposhinda 5-0 mjini Cairo huku michezo mingine ya karibuni Simba ikiwa imeshinda mara mbili na kutoka sare mara mbili.

Kabla ya Simba kutupa karata yao huko Misri, watani wao Yanga watakuwa wageni wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo ni mabingwa wa kombe hilo mwaka 2016 ambapo sare ya magoli ya aina yoyote au ushindi utaivusha Yanga na kutinga nusu fainali ya kwanza ya mashindano ya Afrika. Hatua kubwa ambayo Yanga iliwahi kufikia ni robo fainali mwaka 1969 na mwaka 1970 katika mfumo wa zamani wa mashindano hayo. Mara zote mbili ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana.


Pia Yanga ilifika hatua ya nane bora mwaka 1998 wakati ulipoanzishwa mfumo mpya wa ligi ya mabingwa Afrika.

Mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam ulimalizika kwa sare ya 0-0 huku Mamelodi wakionekana kuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na rekodi yao nzuri wanapocheza nyumbani. Kwa msimu huu Mamelodi Sundowns hawajaruhusu bao lolote wakiwa nyumbani huku Yanga hawajapata ushindi wa aina yoyote ugenini. Yanga inahitaji sare yoyote ya magoli ili kusonga mbele kwa kunufaika na kanuni ya goli la ugeni.


Hata hivyo, Yanga imekuwa na matokeo bora ya michezo ugenini katika michezo ya Afrika hususan msimu uliopita.

Miongoni mwa matokeo bora ya ugenini ni ushindi wa 1-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger japo waliuokosa ubingwa kwa sababu ya kanuni ya goli la ugenini baada ya kukubali kichapo cha 2-1 jijini Dar es Salaam katika mchezo wa mkondo wa kwanza.

Kukosekana kiungo mshambuliaji wa Yanga Rai awa Ivory Coast, Pacome Zouzoua ilikiwa pengo kubwa kwenye mchezo wa nyumbani kwa upande wa Yanga huku akitarajiwa kuanza kwenye mchezo huo wa mkondo wa pili.

Timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwahi kutwaa ubingwa Ligi ya mabingwa Afrika,TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itasafiri mpaka Angola kupambana na Petro de Luanda baada ya sare ya 0-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika mjini Lubumbashi. Mazembe wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya magoli ili kusonga mbele.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI