Header Ads Widget

SERIKALI KUDHAMIRIA KUINUA ZAO LA MWANI

 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imejidhatiti kuinua kilimo cha mwani na mazao ya bahari ili kuwapa tija wakulima na wavuvi hususani Wanawake.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mohammed Said Khamis wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya mwani iliyofanyika katika ukumbi wa mnarani Kisonge.

Kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya mwani inahusisha mikoa zaidi ya mitano Tanzania bara na mikoa yote ya Zanzibar huku ikifadhiliwa na shirika la kimataifa la Maendeleo ya kilimo na uvuvi IFAD kwa mwaka Mmoja.

Amesema kwamba, Serikali ipo katika hatua ya kukamilisha utaratibu wa ujenzi wa kiwanda cha Pili cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe Pemba.

"Tumekamilisha kiwanda cha kwanza cha Kusarifu mwani Pemba na Unguja ambapo kipo katika hatua ya mwisho ya kukamilika kwake na sasa Serikali ipo katika hatua na Utaratibu wa kuanza uhenzi wa kiwanda cha Pili cha kusarifu Mwani na mazao ya bahari," amesema.

"Kukamilika kwa kiwanda ni kulipa thamani zao la mwani na wakulima," ameeleza.

Amefahamisha kuwa, uzinduzi wa program ya uhamasishaji wa zao la mwani hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni muhimu katika kuimarisha sekta hiyo kwa maslahi ya watanzania wote.

Ameongeza kwamba, Serikali kupitia wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi imeona ipo haja ya kuhamasisha matumizi ya mwani ili kulipa thamani zao hilo.

Ameeleza kuwa, kuna tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mwani ni zao pekee lenye virutubisho vingi ukilinganisha na mazao mengi ya baharini hivyo kuna kila sababu kwa wananchi kulithamini zao hilo.

"Ukweli kuwa matumizi ya mwani na bidhaa zake hujenga jamii yenye afya bora na kusababisha kuimarika kwa kinga ndani ya mwili na kuepuka kutumia dawa zisizo na lazima na kuipunguzia serikali gharama za kuagiza dawa," amesema.

Hata hivyo amesema, ili kuhakikisha wanakombolewa wakulima wa zao hilo na kuondokana na hali duni ua kiuchumi wizara imekuwa ikichukua juhudi mbalimbali ikiwemo kuwapatia dhana bora za kilimo ikiwemo boti, utowaji wa taaluma, teknolojia mpya ya ukulima wa zao hilo ili kuleta tija kwa walengwa.

Kwa upande wake mratibu wa shirika la kimataifa la Maendeleo ya kilimo na uvuvi IFAD, Amina Ussi Khamis alisema uzinduzi huo utasaidia kuwainua wakulima wa mazao ya baharini kwa kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao yao na kuinua kipato chao.

Alisema licha ya kulimwa kwa zao hilo kwa kasi kubwa lakini bado kunahitajika jitihada zaidi ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo hivi sasa.

Nae katibu wa ushirika wa Kilimo hai Zanzibar, Semeni Mohammed Salum alisema mwani ni moja ya mazao ya kimkakati hivyo serikali inaungana na wakulima wa zao hilo katika kuwapa elimu ili kuwainua kiuchumi.

"Katika kufikia malengo ya wakulima hao serikali imeandaa mpango wa kuwafundisha wakulima utumiaji wa mbegu bora za mwani ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS