Header Ads Widget

RC BABU AAGIZA KUKAMILIKA KWA UJENZI WA DARAJA LINALOUNGANISHA KATA NNE...



NA WILLIUM PAUL, SAME. 


MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amemuagiza Mkandarasi anayejenga daraja la kuunganisha kata ya Suji, Bwambo, Saweni na Makanya wilayani Same kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Mei mwaka huu ili wananchi waweze kupata huduma hiyo. 


Babu ametoa kauli hiyo alipotembelea kujionea ujenzi wa daraja hilo unaogharimu milioni 399 linalojengwa na kampuni ya Mkandarasi Lenana Holding Company Ltd ambalo linajengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mawe.



Amesema kuwa, wananchi wamekuwa wakipata shida kupita hasa kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea kunyesha  na kumtaka Mkandarasi kuharakisha kukamilisha ili kutatua adha kubwa wanayokumbana nayo wananchi. 


"Mkandarasi umeongezewa muda mpaka mwezi Mei mwaka huu uwe umekamilisha sasa pambana huo mwezi ukifika nataka kuona hiki kivuko kimekamilika na wananchi wanapita sitaki kusikia sababu yoyote na nitakuja mwenyewe kujionea hili" Amesema Babu.


Amesema kuwa, kwa sasa wananchi hawahitaji maneno bali wanahitaji kuona kivuko hicho kikiwa kimekamilika ili waweze kupita muda wote na kuwataka Tarura kumsimamia Mkandarasi huyo ili kukamilisha ujenzi. 


Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara mijini na vijijini (Tarura) wilaya ya Same, Mhandisi James Mnene amesema kuwa, Barabara ya Makanya - Suji - Mweteni inaurefu wa kilomita 25.91 ambapo huudumia kata nne. 



Mhandisi Mnene amesema kuwa, mwaka wa fedha 2023/24 serikali ilitenga fedha milioni 410 ya ujenzi wa kilomita 8 za changarawe na ujenzi wa daraja kwa kutumia teknolojia rahisi ya mawe. 


Amesema kuwa, pia barabara hiyo ilipata fedha za naendelea kutoka mfuko wa bodi ya barabara milioni 600 ambapo itafanyiwa matengenezo ya kilomita 10 kuanzia Suji-Mweteni kwa kiwango cha changarawe. 


Meneja huyo ameongeza kuwa, mradi wa ujenzi wa daraja na urefu wa kilomita 8, ulikusudiwa kukamilika ifikapo Machi 13 mwaka huu lakini kutokana na changamoto ya mvua Mkandarasi aliomba kuongezewa muda na kutakiwa kukamilisha ujenzi ifikapo Mei 13 mwaka huu ambapo kwa sasa mradi umefikia asilimia 80.


Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS