Header Ads Widget

MWENEZI MKOA WA PWANI AAPA KUMSAKA MTENDAJI ALIYE KULA MILIONI 8 ZA UJENZI WA BARABARA

Na Scolastica Msewa, Rufiji



KATIBU wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa  Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani  David  Mramba ameapa kulivalia njuga malalamiko  ambayo yamewasilishwa na Katibu Siasa  na  Uenezi  Kata ya Kibaha Vijijini   Pendo Ernest  juu ya Mtendaji  ambaye anadaiwa kupokea  kiasi cha Mil.8 ili kuziba barabara  iliyoharibika kukaa na fedha hizo mpaka alipohamishwa kituo cha kazi.

Mramba amesema hayo Mlandizi wilayani kibaha mkoani Pwani wakati akitoa mada kwa Makatibu wa Siasa, uenezi na mafunzo wa kata ya kibaha vijijini ambapo Endo amedai kuwa  fedha hizo alikabidhiwa aliyekuwa Mtendaji wao (hakumtaja jina) ambaye hivi sasa amehamishiwa Kata ya Dutumi.

"Tunajua kwamba pesa ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini  kiasi cha Mil.nane lakini kifusi kilichowekwa ni kidogo hivyo kimezalisha tope ambalo hata magari yanashindwa  kupita kutokana na barabara kuzidi kuwa mbovu" amesema.

"Changamoto  iliyojitokeza ni kuharibika kwa kipande cha barabara  hali iliyopelekea Mhe. Mbunge wa Kibaha Vijijini  kutoa Mil.nane ili kuwekwe kifusi lakini hakikuwekwa tumemuuliza Mhe.Diwani ametujibu  kuwa pesa bado ipo lakini hakuna utekelezaji wowote" ameongeza.

 Katibu wa CCM  Tawi la  Mkwajuni  Kata ya Mtambani Kibaha Vijijini Khadija  Ameir Maguto amemueleza Mramba kuwa  wananchi wake wanahitaji utekelezaji  wa barabara ya  Makofia Mzenga Bagamoyo.

"Sisi  viongozi tunapata  malalamiko  mengi kutoka kwa  wananchi  zoezi la ujenzi limeanza miaka mingi lakini hakuna utekelezaji  tuliambiwa kuwa Desemba  mwaka 2023 tutalipwa lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.

Hayo yamejiri leo Aprili 24  katika  ziara ya Mwenezi   Mramba  aliyoipa jina la Ste By Step katika Tarafa ya Mlandizi, Wilaya ya Kibaha vijijini iliyofanyika  katika Ukumbi wa Pentagon uliopo karibu na Stendi Kuu ya magari  Mlandizi.

Aidha katika ziara hiyo,  Mwenezi  wa Mkoa wa Pwani David Mramba  ametoa mafunzo mbalimbali kwa Makatibu wa CCM na Wenezi wa Matawi, Makatibu wa CCM na Wenezi wa Kata za Tarafa hiyo na Makatibu wa Hamasa wa Kata hizo.

Aidha mafunzo mengine yaliyotolewa ni  suala zima la  Itifaki ya ukaaji, Itifaki ya bendera, Itifaki ya magari na Itifaki ya Mavazi, Uongozi na Maadili  elimu iliyotolewa na Katibu wa Vijana Kibaha Vijijini Jacob Kituu.

Aidha Mramba   amewasisitiza wanachama kuendelea kuheshimiana, kuthaminiana, na kusaidiana ili kufikia malengo ya Chama CCM

Amesema ni wajibu wa kila mwanachama kulipa ada na kujitoa ndani ya chama huku akiwataka kutimiza majukumu yao kutokana na Katiba ya CCM inavyoeleza.

Amewataka wanachama wa CCM Kibaha Vijijini kuwa wamoja ili waweze  kukijenga chama na kujiandaa  na mikakati madhubuti  katika kuelekea chaguzi zilizopo mbele yao ambazo ni  uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, Vitongoji, na 2025 uchaguzi Mkuu.

Amewakumbusha kuwa nafasi walizo nazo ni dhamana hivyo wanatakiwa kuzitumia kwa maslahi ya Chama na si kwa maslahi
yao binafsi.

Aidha amewakemea baadhi ya wanachama kuanza kuandaa wagombea kabla ya muda wa uchaguzi jambo ambalo linatengeneza nakundi na kukigawa chama.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS