Header Ads Widget

MBUNGE MBEYA VIJIJINI AKABIDHI AMBULANCE KWA HOSPITALI YA WILAYA YA MBEYA, WANANCHI WASHUKURU

 .



NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Mbunge wa Jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amekabidhi gari la wagonjwa (Ambulance) kwa uongozi wa Wilaya ya Mbeya ili kusaidia kuboresha huduma za afya katika Wilaya hiyo.


Mbunge Njeza amekabidhi gari hilo kutoka Serikali kuu mbele ya wananchi wa Kata ya Inyala kwa niaba ya wananchi wa Mbeya vijijini ambapo ameelekeza shukrani zake kwa Serikali kwani karibia kila Wilaya imepata gari la wagonjwa lakini kwa Wilaya ya Mbeya imepata zaidi ya gari moja.


Kwenye mapokezi ya gari hilo la wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbeya iliyoko Inyala Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya amesema utekelezwaji wa miradi hiyo ya kimaendeleo unatokana na uwajibikaji mzuri wa wananchi kwenye ulipaji kodi kwa maendeleo ya Taifa lao.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya Paul Mamba Sweya, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza kwa kuendelea kupambana kuhakikisha Jimbo hilo linapata fedha na raslimali mbalimbali ikiwemo usafiri wa gari la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mbeya.


Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Sebastian Mwalupindi, amesema CCM inaridhika na utekelezwaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo ikiwemo kwenye sekta ya afya ambapo gari hilo la wagonjwa linakwenda kuboresha utolewaji huduma kwa wananchi.


Mwenyekiti huyo amesema kutokana na mambo yanavyotafsiriwa kwa vitendo ni wazi kwamba CCM inakwenda kushinda kwa kishindo kwenye chaguzi zijazo.


Diwani wa Kata ya Inyala Mwalingo Kisemba amesema muunganiko uliopo kati ya viongozi wa Wilaya Jimbo na ngazi nyinginezo ndio zimesaidia kuchochea upatikanaji miradi mingi ya fedha hususani Mbunge Njeza ambaye ni kiungo muhimu kupitia kuwa kwenye Kamati ya bajeti na fedha bungeni.


Wananchi wa Mbeya vijijini wameshukuru Serikali kwa kutoa gari hilo ili kurahisisha utolewaji wa huduma za kiafya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI