Na Hamida Ramadan, Matukio Daima App Dodoma
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeandaa Marathon ambapo jumla ya shilingi Bilioni 3 zinatarajiwa kukusanywa na kujengwa shule ya wavulana pamoja na viwanja vya michezo vya kuendeleza vipaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9,2024 Bungeni Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bunge Marathon ambaye ni Mbunge wa Makete Festo Sanga amesema zoezi la usajili linaendelea katika Vituo mbalimbali kwa kiasi cha Shilingi elfu 40 ambapo kupitia mbio hizo mshindi wa kwanza anatarajiwa kujikusanyia kitita cha Fedha za kitanzania Shilingi Milioni Tano.
Amesema Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika 13 April Jijini Dodoma katika viwanja vya Jamhuri ambapo watu mbalimbali watashiriki wakiwemo Wabunge wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt,Tulia Ackson.
"Marathon yetu ni mawazo ya mheshimiwa Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson na inafanyika kwa mara ya kwanza ikiwa ni moja kati ya mikakati yetu kutafuta fedha kwaajili ya kujenga shule ya wavulana ya Bunge Boys Sekondari, kwa sababu pia tumeshawekeza nguvu kwa wasichana katika sekta ya Elimu, tumeona pia kufuata maono ya Mheshimiwa Rais ya kuinua Elimu pia hata kwa mtoto wa kiume kwa kujenga Shule maalum kwaajili ya watoto wa kiume” Amesema Festo Sanga.
Na kuongeza "Kuhusu zoezi la Usajili Sanga amesema mpaka sasa Taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi zimeendelea kujisajili, pia wakimbiaji maarufu ambao wako nchini nao wameonesha ushirikiano na wanatarajiwa kushiriki huku mshindi wa kwanza atapata Kiasi cha Shilingi Milioni Tano, " Amesema.
Aidha amebainisha kuwa Marathon sio ya Bunge pekee bali ni ya watanzania wote, kwani zipo zawadi zilizoandaliwa na mshindi wa kwanza atapata Shilingi milioni tano kwa Km 21, pia kuna zawadi ya Mshindi wa pili na kuna zawadi ya Mshindi wa Tatu, kuna Km 10 tunaenda kutoa Milioni 3, lakini pia kuna Km 5, mkimbiaji anaenda kupata Milioni Moja na Laki Tano.
"Niwaombe watanzania kupitia Taasisi na Kampuni binafsi kuunga mkono juhudi hizo za kujenga Shule ikiwemo kutoa Vifaa vya Ujenzi ambapo pia amezishukuru baadhi ya Taasisi ambazo zimeshatoa Vifaa kama sehemu ya kusapoti, " Amesema
Hata hivyo Vituo vya Usajili vinapatikana katika Mikoa ya Dar es salaam na Dodoma ambapo kwa Dar es salaam ni katika Ofisi za Bunge, Mlimani City na Dodoma ni Shoppers Plaza, Jamhuri, Safina House pamoja na Bungeni.
0 Comments