Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wakuu wa idara na watendaji wa Serikali katika Halmashauri za mkoa Kigoma wametakiwa kusimamia kikamilifu mpango wa ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji wa miradi ili kuwafaanya wananchi hao kuwa sehemu ya miradi hiyo na kuifanya miradi kuwa endelevu badala ya kufanyiwa hujuma.
Mshauri wa elimu kutika ubalozi wa Uingereza nchini, Dk. John Lusingu alisema hayo kwenye ziara ya kukagua na kufanya tathmini ya hali ya utekelezaji mradi wa Shule Bora Mkoani Kigoma ili kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa mambo yaliyomo kwenye mradi huo.
Dkt. Lusingu alisema kuwa ushirikishwaji kamili wa wananchi kwenye miradi hiyo hasa inayotekelezwa kwa fedha za wafadhili inajenga taswira ya wananchi kuiona miradi hiyo kuwa ni ya kwao na hivyo kushiriki kuitekeleza, kuilinda na kuitunza hivyo miradi hiyo inakuwa na tija kubwa kwa wananchi kwa muda mrefu.
Akiwa wilayani Buhigwe Mshauri huyo alishuhudia mafanikio makubwa katika baadhi ya shule alizotembelea ikiwa ni pamoja na kuibuliwa kwa shughuli za uzalishaji mali ikiwemo upandaji wa miti kwa ajili ya miradi ya shule ambapo kwa sasa baadhi ya shule zimeanza kuvuna miti hiyo na fedha zilizopatikana zimeanzisha miradi mingine.
Baadhi ya mafanikio aliyoshuhudia kwenye ziara hiyo ni Pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu miradi inayotokana na fedha za upandaji miti, baadhi ya shule kuanzisha kilimo cha Kahawa, ufugaji wa Nyuki,ufugaji kuku na miradi mingineyo ambayo imezifanya shule zilizo kwenye mradi huo kuwa na vyanzo vya mapato.
Akitoa ushuhuda kwa Mshauri huyo wa elimu wa Ubalozi wa Uingereza nchini na ujumbe aliofuatana nao, Mwalim Mkuu wa shule ya Msingi Mkatanga, Judith Ndiga alisema kuwa kupitia program ya UWAWA inayotekelezwa kupitia mradi wa shule bora wamefanikiwa kuanzisha utaratibu wa kudumu wa kutoa chakula kwa wanafunzi katika shule hiyo jambo linalosaidia kuongeza ufanisi kitaaluma na kupunguza utoro.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnyegera iliyopo, Fidel Ernest alisema kuwa mara baada ya kuanza utekelezaji wa programu ya Mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) hali ya kujiamini kwa walimu kwenye kufundisha imeongezeka sambamba na uwepo wa ongezeko la ufaulu kwa shule hiyo hadi kufikia zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi wa darasa la saba kwa mwaka 2023 shuleni hapo.
Mwalimu Ernest amebainisha kuwa maboresho makubwa ya miundo mbinu ya kielimu yanayofanywa na serikali kupitia mradi wa Shule Bora yameendelea kuyafanya mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kuwa rafiki kwa walimu sambamba na wanafunzi hali inayoendelea kuimarisha utoaji wa elimu bora.
Mwisho
0 Comments