Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
WIZARA ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,imewagiza watendaji wa vijiji,kata na mitaa katika halmashuri zote nchini kuliweka katika agenda ya kudumu kwenye vikao vya Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) suala la anwani ya makazi ili kuweka uendelevu wa usimamizi na uhakiki wa taarifa za anuani za makazi.
Mtaalamu wa Mfumo wa anwani ya makazi kutoka wizara hiyo, Innocent Jacob, alisema hayo jana wakati wa mafunzo ya siku mbili ya Uhakiki Anwani za Makazi katika Mfumo wa Kidigitali (NaPA).
Mafunzo hayo yanatolewa kwa watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa ajili ya uhakiki wa anwani za makazi.
Jacob alisema anwani za makazi ni muhimu sana kwasababu zinasaidia ulinzi na usalama,kutoa huduma kwa wakazi na pia inasaidia biashara mtandao kupitia fumo wa Kidigitali (NaPA).
"Anwani za makazi ni miundombinu ya mawasiliano inayorahisisha utambuzi wa mtu alipo au mtu stahiki alipo aidha mahali pa kazi biashara au ofisi aweze kupata huduma kwa urahisi," alisema.
Jacob alisema mfunzo kwa viongozi hao yanatolewa ili kuwawezesha kwenda kuhakiki taarifa za wakazi wao katika maeneo yao ya kiutawala ambapo zoezi hili la uhakiki wa anwani za makazi katika awamu ya kwanza linafanyika katika Manispaa za Singida,Iringa na Kigoma na baadaye litafanyika nchi nzima.
"Tunafahamu mfano katika Manispaa ya Singida kuna kata18 na mitaa 72 kwa hiyo tunataka kuona wakazi wanahakikiwa taarifa zao kwani wapo ambao baadhi ya taarifa hazikuingizwa kwenye mfumo kipindi zoezi hilo lilipofanyika,"alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Adrianus Kalekezi akifungua mafunzo hayo alisema uwepo wa anwani za makazi utakuwa msaada mkubwa kwa jamii kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea.
"Hizi Anwani za Makazi ni maagizo kutoka kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba nchi nzima twende kwenye Anwani za Makazi na zoezi hili lilianza tangu huko nyuma.
"Uwepo wa Anwani za Makazi kuna faida kubwa jambo ambalo litakuwa msaada kwa wakazi na nchi yetu kwa ujumla kama ambavyo wetu Ulaya wamekuwa na utaratibu huu ambao umekuwa ni rafiki, haa tunapewa elimu zaidi, ilikwenda katika Kata, Mitaa na Vijiji vyetu kuona mambo yanaenda sawa kwa kuwa na Anwani za Makazi, lakini pia mafunzo haya yatajenga uelewa hasa katika Mfumo wa kidigitali(NaPA)," alisema.
0 Comments