Header Ads Widget

UJENZI VYUO VIPYA VYA VETA KATIKA WILAYA 64 KUONGEZA UDAHILI WANAFUNZI KUFIKIA 140,000



Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA


MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema ujenzi unaoendelea wa vyuo 65 katika wilaya 64 na kimoja cha mkoa utakapokamilika utaifanya mamlaka hiyo kuwa na jumla ya vyuo 145 nchini na hivyo kuongeza udahili wa wanafunzi ambao watafikia  zaidi ya 140,000.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema hayo jana (Machi 28, 2024) wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilitembelea kuangalia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi (Ikungi DVTC) mkoani Singida.



"Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 serikali ilitenga Sh.bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika wilaya 64 na chuo kimoja cha ufundi stadi na huduma cha Mkoa wa Songwe ujenzi wa vyuo hivyo unalenga kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo angalau kimoja cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi," alisema Kasore.


Kasore alisema ujenzi zaidi wa vyuo vya VETA na udahili wa wanafunzi kuongezeka utaongeza uwezo wa wananchi kupata ujuzi katika  shughuli mbalimbali za uchumi hasa ikizingatia kuwa VETA imeanza kuimarisha mitaala ili iweze kuendana na mahitaji ya soko la ajira.



"VETA tunatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu aliona kuna suala zima la wananchi kupata ujuzi ili waweze kushiriki vyema katika shughuli za kiuchumi na kitekeleza miradi ya kimkakati, hivyo aliona ni vyema kuwepo na vyuo vya VETA vya kutosha," alisema Kasore.


Alisema suala la kufanya mabadiliko katika sera ya elimu na mitaala ni eneo ambalo VETA imejikita kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi kuanzia shule za awali,msingi,sekondari na katika vyuo.



Kasore alisema ujenzi wa Chuo cha VETA Ikungi ni miongoni mwa ujenzi wa vyuo 25 hapa nchini ambao utekelezaji wake ulianza 2020 mradi ambao umefadhiriwa na kutolewa fedha na serikali ambapo yamejengwa jumla ya majengo 17.


Aliongeza kuwa ujenzi wa chuo hicho umegharimu Sh.bilioni 3.004 ambapo ujenzi pekee yake ni Sh.bilioni 2.6 na uwekaji wa samani za ofisini,madarasani,mabweni,bwalo na kwenye katakana zimetumika Sh.milioni 350.



Alisema chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 240 wa kozi za muda mrefu kati yao 144 wa bweni na 96 wa kutwa na pia kinaweza kudahili wanafunzi takribani 700 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka kwa kuzingatia mahitaji ya shughuli za kiuchumi za Wilaya ya Ikungi na maeneo ya jirani.


"Katika mwaka huu wa masomo (2024) chuo kimeanza kutoa mafunzo ya muda mrefu ambayo yameanza mwezi Januari na hadi kufikia Machi 28, 2024 kimedahili wanafunzi 45 kati yao 30 ni wa fani ya ufundi wa umeme na 15 wa fani ya ushonaji," alisema Kasore.



Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia, Prof Carolyne Nombo, alisema serikali imedhamiria kutoa ujuzi kwa vijana wa kitanzania kupitia taasisi ya VETA  au katika sekondari chache ambazo zimeanza kutoa mafunzo kwa kutumia mitaala ya VETA.


"Serikali hivi sasa suala la ujuzi ndio mpango mzima,kuanzia mwaka huu shule 28 za sekondari za serikali na 68 za binafsi zimeanza kutoa mafunzo kwa kutumia mitaala ya VETA ambapo taaluma zinazotolewa zinaendana na upatikanaji wa soko la ajira katika maeneo husika," alisema.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga aliitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kufanya mageuzi katika vyuo kwa kuweka mkakati wa kuwasaidia wabunifu ili taifa liweze kupata wataalam wa kutosha na hivyo kufikia azma ya sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kujenga nchi ya viwanda.



Alisema ili nchi iweze kusonga mbele wabunifu wanahitajika kinachotakiwa ni kuwasaidia kwani huko nyuma kulikuwa na upungufu wa wataalam na ndio maana serikali imejenga vyuo vya VETA wafundishwe ili waende kwenye viwanda.


"Kule mkoani kwangu (Songwe) kuna kijana wa darasa la saba alitengeneza chopa na anairusha hadi juu lakini changamoto akitaka kuishusha inabidi aizime kwanza ndipo adondoke nayo,sasa VETA ingeweza kumsaidia huyu mbunifu," alisema Hasunga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe.



Hasunga alisema kamati ilikwenda mkoani Mwanza na kujionea watanzania walivyounda meli yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo, hivyo kila kitu kinawezekana kinachohitajika ni dhamira ya kweli ya kuwawezesha na kuwasimamia Watanzania wanaweza.


Naye Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe,alisema tatizo kubwa vijana hawatengenezwi kubobea katika masuala fulani ya ufundi jambo ambalo wakiingia kwenye soko la ajira wanashindwa.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS