Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Charles Gombo (mwenye kofia kulia) akitoa maelekezo kwa vitendo kuhusu mpango wa uboreshaji wa uandikishaji wa anuani za makazi katika manispaa ya Kigoma Ujiji
Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Charles Gombo (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa vitendo kuhusu mpango wa uboreshaji wa uandikishaji wa anuani za makazi katika manispaa ya Kigoma Ujiji
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SERIKALI imewataka watendaji wa mitaa,vijiji na kata kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kuhusika na uharibifu wa anuani za makazi mpango uliotekelezwa na serikali.
Katibu Tawala wa wilaya Kigoma,Mganwa Nzota alisema hayo katika mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa mitaa na kata wa manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa ni utekelezaji wa marekebisho na maboresho ya mfumo wa anwani za makazi mafunzo yanayotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Nzota alisema kuwa serikali imetumia gharama kubwa katika utekelezaji wa mpango huo ili kurahisisha upatikanaji kwa urahisi wa watu na ofisi na kwamba haitavumilia kuona miundo mbinu iliyowekwa kwa ajili ya mpango huo inaharibiwa.
Akizungumzia mafunzo hayo na utekelezaji wa mpango huo Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Charles Gombo alisema kuwa kwa sasa wanafanya zoezi la kusasisha taarifa na miundombinu iliyofanyika kwa kipindi kilichopita sambamba na kuhuisha na kukusanya taarifa mpya.
Mtaalam huyo alisema kuwa zoezi hilo la uhakiki wa taarifa utafanyika kwa siku 12 ukihussisha ukishirikisha viongozi kutoka kata 19 na mitaa 68 ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Utambuzi na uwekaji wa Anwani za makazi Nchini ulifanyika na unafanyika kwa kutoa namba ya anwani (namba ya jengo, au kiwanja), majina ya barabara au kitongoji na postikodi ili kuweza kila Mtanzania kuwa na anwani halisi ya Makazi yatakayosaidia kila mtu kupatikana kirahisi, utambulisho wa watu, usajili wa biashara, kufanyika kwa biashara mtandaoni ambapo Wafanyabiashara na wanunuzi watakuwa na uwezo wa kununua na kumfikishia mteja bidhaa, upatikanaji wa huduma za dharura kama vile polisi, na huduma za zima moto.
0 Comments