Na Thobias Mwanakatwe, MANYONI
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Manyoni mkoani Singida, Barnabas Mushi amepiga marufuku wafugaji kugeuza maeneo ya taasisi za serikali kuwa sehemu za malisho ya mifugo yao.
Aidha, ameagiza mifugo itakayokamatwa ikila miti iliyopandwa ikamatwe na kugawiwa kwa taasisi (shule) husika na wanafunzi wachinjiwe nyama ili kupoza machungu ya miti yao kuliwa.
Alisema hayo juzi wakati wa zoezi la upandaji miti kuzunguka katika Shule ya Sekondari Sasilo iliyopo Tarafa ya Nkonko wilayani hapa kwa ajili ya kuhifadhi mazingira ya shule hiyo.
Katika zoezi hilo ambalo limefanywa na jumuiya hiyo jumla ya miti 3,780 imepandwa katika maeneo ya taasisi ya tarafa ya Nkonko kwenye kata za Nkonko, Isseke, Sanza, Sasilo, Heka na Chikola.
Mushi alisema ili kutunza miti inayopandwa isiharibiwe na nifugo aliwaomba watendaji wa vijiji na kata kukamata mifugo hiyo inayofanya uharibifu kwenye taasis na kuigawa kwa taasisi husika.
"Niwaombe watendaji ukishika mbuzi imekula miti kama ni miti ya shule wape wanafunzi mbuzi huyo wamle wapunguze uchungu wa utunzaji na uhifadhi mazingira maana tukichekeana tutapoteza miti na tutakuwa na jangwa kisha tutaanza kuulizana kwanini atuna mvua," alisema.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi alisema moja ya majukumu ya jumuiya hiyo ni kusimamia afya, elimu, malezi, mazingirna utamaduni hivyo ni jukumu la kila mwananchi kutunza mazingira ili yawatutunze.
Mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizindua zoezi la upandaji miti katika wilaya zote za mkoa huu aliagiza Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani kuhakikisha wanatunga sheria kali zitakazowafanya wafugaji kuwa makini na mifugo yao sambamba na kuweka faini kubwa kwa atakaye sababisha mfugo kula miti.
Aidha,Serukamba alitoa maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri a Mkurugenzi kuhakikisha wananchi wanapunguza tabia ya ukataji miti hovyo na uchomaji wa mkaa.
Asilimia kubwa ya miti iliyopandwa wakati wa kampeni ya upandaji miti kandokando ya barabara kuu ya Manyoni-Singida imekufa kutokana na kuliwa na mifugo.
MWISHO
0 Comments