Header Ads Widget

MTOTO WA MIEZI MINNE AUAWA KWA KUPIGWA NA FIMBO KICHWANI, BABA NA MAMA WAKIGOMBANA

 


Na Moses Ng’wat,Songwe.


JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linamtafuta, Masumbula Nemson, Mkazi wa Kitongoji C  katika kijiji cha Namkukwe, Wilayani Songwe kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wa miezi mine baada ya ugomvi na mke wake. 


Nemson anadaiwa kumuua mtoto wake huyo wa miezi minne, Blasto Nemson, kwa kumpiga na fimbo kichwani upande wa kulia akiwa mgongoni mwa mama yake.


Ugomvi huo unaohusisha wivu wa mapenzi, unadaiwa kuibuka baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mkewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.


Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Machi 8, 2024 majira ya saa 2:00 usiku na kwamba baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho alitorokea kusikojulikana.


“Upelelezi unaoambatana na msako mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa na pindi akikamatwa atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria” alisema Kamanda Mallya.


Aidha, Kamanda Mallya alisema katika tukio hilo, pia mama wa marehemu alijeruhiwa kichwani na mikono yake yote miwili wakati akijikinga na kumkinga mtoto wakiwa wanashambuliwa kwa fimbo na mtuhumiwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI