Header Ads Widget

SERIKALI KARAGWE KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO

 


Na Shemsa Mussa,Kagera 

     

Mkuu wa wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera Julius Kalanga Laizer amesema Serikali Wilayani humo haitofumbua macho vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinavyofanyika katika jamii na kusababisha madhara makubwa huku akieleza kupambana kwa njia yoyote ile ili kukomesha hali hiyo.


Dc Laizer alitoa kauli hiyo Machi 8, 2024 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Mjerumani uliopo wilayani Karagwe  Kufuatia zaidi ya watoto 25 kufanyiwa vitendo vya ubakaji kupitia taarifa ya Afisa ustawi wa jamii aliyoitoa mbele ya kiongozi huyo.


Dc Laizer alisema kuwa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinazidi kuongeza na kuwa serikali haitawafumbia macho wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.


kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka Wananchi kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika maeneo yao ili serikali kwa kishirikiana na Wananchi waweze kukomesha vitendo hivyo  kuanzia ngazi ya familia ,jamii na taifa kwa ujumla


Aidha akieleza hali ya vitendo hivyo Afisa Ustawi wa Jamii Wilayani humo Owokusima Kaihula alisema kuwa hali ya usalama kwa watoto katika wilaya ya Karagwe sio nzuri kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji kwa watoto hususani kuanzia miaka 3 hadi 15.


Alisema kuwa zaidi ya Watoto 25 walifanyiwa vitendo vya ubakaji kuanzia mwezi Januari hadi Machi  2024 na kuwa hali hiyo imesababishwa na Wanawake walio wengi  au Wazazi kujisahau katika majukumuu yao ya malezi kwani wengi wao wamekuwa bize na kutafuta pesa bila kujua watoto wao wako wapi na wanafanya kitu gani.


Bi Kaihula aliwataka Wazazi kubadilika na kurudi katika malezi ya zamani kwa Watoto wao jambo litakalosaidia kupunguza vitendo hivyo vya ubakaji,huku akiwakumbusha kuwaombea watoto kwa Mwenyezi Mungu kila wakati.


Kwa upande wao Wanawake wamekiri wengi wao kujikita katika shughuli za uzalishaji na kusahau majukumu yao katika malezi na makuzi ya watoto wao.


Ikumbukwe kuwa Maadhimisho hayo Kimkoa yamefanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa Uhuru(Mayunga) huku  mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa ambapo pia yamebeba kauli mbiu isemayo WEKEZA KWA MWANAMKE KUHARAKISHA MAENDELEO YA TAIFA NA USTAWI WA JAMII

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI