Header Ads Widget

ANDENGENYE AKEMEA MATUMIZI YA PESA KUNUNUA HAKI ZA WANAWAKE

 


Na  Fadhili Abdallah,Kigoma

 

 

Mkuu wa mkoa Kigoma  Thobias Andengenye ameitaka jamii kukataa tabia ya watu wenye uwezo wa kiuchumi na fedha kupora haki za wanawake na Watoto kwenye mashauri mbalimbali yanayojitokeza dhidi yao ikiwemo unyanyasaji kingono na masuala ya kumiliki mali.

 

Andengenye alisema hayo katika Kijiji cha Makere wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma  alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya mkoa huo ya siku ya wanawake duniani na kubainisha kuwa bado haki za wanawake na Watoto zimekuwa zikikiukwa kwa misingi ya kuwapendelea watu wenye uwezo kiuchumi.

 

Mkuu huyo wa mkoa amepinga vitendo vya ukatili kwa wasichana na Watoto ikiwemo kukatishwa masomo na kuozwa kwa wanaume wenye uwezo wa kifedha, wanaotoa ng’ombe nyingi mambo ambayo yanakatisha ndoto za wasichana hao na hivyo kutaka taarifa za vitendo vya ukatili zisifichwe au kumaliza mashauri kwenye ngazi ya familia.

 

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali itaendelea kutekeleza maazimio ya Beijing, mpango wa maendeleo ya Taifa na mkakati wa serikali katika kuongeza kipato na kuinua uchumi wa wanawake ili kuwafanya wanawake kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na katika kuondoa umasikini nchini.


Akisoma risala kwa niaba ya makundi mbalimbali ya wanawake yaliyohudhuria maadhimisho hayo, Zuwena Hussein alisema kuwa kusimamishwa kwa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum kumekuwa na athari kubwa katika kuwafanya wanawake na wasichana kujikwamua na umasikini.

 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuia ya wanawake wa CCM mkoa Kigoma (UWT),Agripina Buyogera alisema kuwa bado vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kingono havijachukuliwa kwa unaostahili na kuendelea kuathiri maisha ya wanawake na wasichana mkoani Kigoma hivyo kuitaka serikali na vyombo vyake kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo.


Aidha Buyogera alisema kuwa serikali haina budi kurudisha mikopo kwa makundi maalum wakiwemo wanawake inayotolewa na halmashauri kwani mikopo hiyo imekua na mchango mkubwa katika kuinua uchumi na kipato cha wanawake na hivyo kuwafanya waondoke na utegemezi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI