Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati Dunia ikiwa kwenye wiki ya Mwanamke inayotarajiwa kufikia tamati Machi 8 mwaka huu,baadhi ya wanawake katika kata ya Kifanya halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe wamelalamikiwa kuwapo kwa ukatili ndani ya familia pamoja na mateso juu ya mikopo kausha damu.
Katika maadhimisho ya siku ya Mwanamke yaliyofanyika katika kata ya Kifanya baadhi ya wanawake hao akiwemo Fausta Mtewele na Joyce Mpogole wanasema bado ukatili ndani ya familia unawatesa katika kujitafutia kipato huku wakilalamikia mikopo Kausha damu kwani baadhi ya familia zimesambalatika na kuwatelekeza watoto kutokana na kudaiwa marejesho yenye riba kubwa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la wanawake halmashauri ya mji wa Njombe Happy Mng'ong'o mbali na kueleza namna wanavyotatua changamoto za wanawake lakini anawataka kupendana wenyewe kwa wenyewe kwani masengenyo,Umbea na hata fitina zimekuwa chanzo cha kuvuruga ndoa.
Diwani wa kata ya Kifanya Nolasko Mtewele anakiri kuwa wanawake wamekuwa muhimu katika familia kwani Wanaume pekee yao hawawezi kufanya vizuri katika masuala mengi kauli iliyoungwa mkono na Angela Mwangeni Diwani wa viti maalum tarafa ya Njombe mjini na Mlezi wa Kata ya Kifanya.
Kwa upande wake mgeni wa heshima katika Maadhimisho hayo Erasto Mpete Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe anasema serikali inaendelea kuwapambania wanawake katika nyanja za kiuchumi,Kisiasa na hata kupambana na ukatili wa kijinsia hivyo wanapaswa kumuunga mkono Mwanamke mwenzao Dokta Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Mpete ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kurejesha mikopo ya 10% iliyokuwa ikitolewa kwenye makundi ya Wanawake,Vijana na Walemavu kwani malalamiko yamekuwa ni makubwa hasa kwa wanawake ambao wameanza kukimbia ndoa zao kutokana na Mikopo kausha damu.
Kauli mbiu ya siku ya wanawake kwa mwaka 2024 Inasema''Wekeza kwa mwanamke kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii''.
0 Comments