Na; Kiobya (shamteabas@gmail.com)
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la Pili) iliyochapishwa na Oxford University Press, mwaka 2004, inafasili kwamba "donda ndugu" ni donda lisilotibika!
Sasa, je, milipuko ya uhaba wa sukari nchini imekuwa donda ndugu?
Tangu tupate uhuru, takriban miaka sitini (60) iliyopita, mawaziri ambao waliwahi kuwajibishwa ama kujiwajibisha (kwa nyakati tofauti) kutokana na milipuko ya uhaba wa sukari ni: Joseph Mungai, Ibrahim Kaduma, John Malecela na Idd Simba. Hayo yalitokea zaidi ya miaka kumi na mitano iliyopita, kisa: uhaba wa sukari! Ni kisa kinachojirudia; kwa nini? Pengine tujiaminishe ya kuwa ni donda lisilotibika, donda ndugu. Donda ambalo, kwa waswahili, hutokana na mkono wa mtu (mikono ya watu!).
Mara kwa mara hapa nchini, kuanzia mwezi Novemba mpaka mwezi Aprili, hujitokeza uhaba wa sukari. Hali hii husababisha bidhaa hii kuuzwa kwa bei ya juu ambayo, kwa walio wengi, hushindwa kuimudu.
Kipindi hiki (kati ya Novemba na Aprili) kinajulikana vizuri, hasa kwa wazalishaji wa sukari nchini. Aidha, kinajulikana hata kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na sukari nchini. Ni kipindi kinachoambatana na masika. Katika kipindi hiki uzalishaji hupungua kwa sababu ya mvua kuwa nyingi. Mvua husababisha mashamba ya miwa kujaa maji na kufanya uvunaji wa miwa kuwa mgumu au wakati mwingine kusitishwa. Kutokana na uzoefu huu, wafanyabiashara hutumia kipindi hiki "vyema" kujineemesha. Hufanya maandalizi mapema kwa kulimbikiza akiba (stock) ya sukari wakisubiri iadimike, kisha waiuze kwa kupanga bei wanavyotaka.
Mathalan, bei za mwaka huu zimetia fora! Bei ya sukari imepaa kutoka wastani wa Sh.1,800 mpaka zaidi ya Sh.6,000 kwa kila kilo. Mfano halisi ni katika Manispaa ya Bukoba ambapo bei ya sukari kwa sasa ni Sh.4,000 hadi 4,500. Walakini, ikumbukwe kwamba Manispaa hiyo ipo karibu na kiwanda cha sukari kinachoitwa "Kagera Sugar". Kuna umbali usiozidi kilomita hamsini (50) tu. Bei ya sukari katika Manispaa ya Bukoba inasawiri "udonda ndugu" wa kitendawili cha uhaba wake. Sukari huzalishwa mkoani Kagera, karibu na mpaka wa Tanzania na Uganda. Kutoka huko husafirishwa mpaka kwa wakala, Mwanza mjini, ambaye hurudisha sukari hiyo mkoani Kagera, ili iuzwe! Kwa mzunguko huo, hata kama hakuna uhaba, lazima bei kwa mlaji iongezeke. Hilo ni jambo mojawapo la mauzauza ya bei ya sukari, hasa mkoani Kagera.
Wenye dhamana ya bidhaa hii wapo na wanajua fika sera ya kulinda viwanda nchini. Hata hivyo, hawajishughulishi kushauri serikali kurekebisha sera iliyopo kwa manufaa ya walaji (wananchi) na wazalishaji. Lengo la sera ni kuvikuza na kuvilinda viwanda vya sukari nchini dhidi ya ushindani kutoka nje. Lakini pale uzalishaji usipokidhi matakwa, wenye viwanda vya sukari wanawajibika kuagiza bidhaa hii nje ya nchi kwa minajili ya kuziba pengo. Ijapokuwa viwanda vya kuzalisha sukari nchini vimekuwa vikiongezeka, bado kinachozalishwa hakijaweza kukidhi mahitaji. Mpaka sasa kuna viwanda sita: Kilombero (Morogoro), Mtibwa Sugar Estate Limited (Morogoro), TPC (Kilimanjaro), Kagera Sugar Limited (Kagera), Bakhresa Sugar Limited (Bagamoyo, Pwani) na Mukulazi Holding Company Limited (Morogoro). Vyote kwa pamoja vilitarajiwa hadi mwaka 2024 kuzalisha tani laki 6.7, lakini lengo hilo limeshindikana. Yaani havijaweza kukidhi mahitaji. Sera iliyopo inavilazimu kuagiza sukari kutoka nje ya nchi ili kuondoa nakisi. Takwa hili hupuuzwa, na wenye dhamana ya kusimamia utekelezaji nao hupuuza! Matokeo ya yote mawili, ni milipuko ya uhaba wa sukari nchini.
Hoja ni kwamba pamoja na kuwepo fursa ya kisera ya kuangiza sukari mapema ili kuziba pengo linalojulikana kwa wazalishaji wa sukari nchini, kwa nini takwa hilo halitekelezwi? Ni kwa manufaa ya nani, au kumkomoa nani? Iweje hali hii ijirudie kila mwaka? Taswira inayojitokeza ni masilahi binafsi! Milipuko ya uhaba wa sukari ni fursa kwa wasimamizi wa sera tajwa, wafanyabiashara wa sukari, wakishirikiana na wenye viwanda. Kama viinimacho, yanatolewa matamko ya kuzuga na kupanga bei elekezi zisizotekelezeka! Kwa waswahili, huo ndio mkono wa mtu (mikono ya watu!).
Hii hali inaweza kunasibishwa na kisa katika kitabu kiitwacho "THE MERCHANT OF VENICE" - 1596 (Mfanyabiashara wa Venice) kilichoandikwa na SHAKESPEARE. Mhusika mkuu katika kitabu tajwa ni *Shylock*, mfanyabiashara bepari na katiri, mwenye uchu wa mali na "*maokoto*". Shylock aliingia katika mkataba wa hila na mshindani wake kibiashara, *Antonio*, ili hatimaye aweze kumuua. Shylock alijua kwamba Antonio asingeweza kurejesha mkopo pamoja na riba. Alichotarajia ni kuwa angeshindwa kutimiza makubaliano kulingana na mkataba, na maisha yake yangekuwa hatarini. Mkataba ulikuwa bayana kwamba akishindwa kulipa mkopo na riba, kikatwe kipande cha nyama chenye uzito wa kilo moja kutoka kwenye eneo la moyo wake. Antonio alinusurika kwa kusaidiwa na hakimu mwerevu ambaye alimtaka Shylock kukata kipande cha kilo moja ya nyama bila tone la damu kudondoka! Sharti la kutodondoka hata tone moja la damu, halikuwa kwenye mkataba huo haramu kati yao! Hakimu alifinyanga sharti hilo kwa minajili ya kuokoa maisha ya Antonio.
Kwa muktadha wa mfano wa simulizi hii, serikali inapaswa "kufinyanga" upya sera ya kulinda viwanda na uwekezaji nchini. Ihakikishe viwanda vinavyozalisha sukari vinaagiza nakisi ya mahitaji katika muda mwafaka, bila visingizio. Hatua hiyo itanusuru wananchi kuondokana na adha ya karibu kila kipindi fulani kukosa bidhaa muhimu za vyakula kama sukari na mafuta ya kula. Huenda huo utakuwa mwarubaini kuntu wa donda ndugu
0 Comments