Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kusimamia miradi yote ya ujenzi na matengenezo ya barabara inayotekelezwa mkoani hapa ili ikamilike kwa wakati na thamani ya fedha iweze kuonekana.
Alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja inayoendelea kutekelezwa katika wilaya za Iramba na Mkalama.
Serukamba alisema serikaki imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuiunganisha miji kwa lami hivyo ni wajibu wa viongozi wote kushirikiana kuisimamia ijengwe vizuri ili ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.
Serukamba pia aliiagiza TARURA kuomba fedha serikalini kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika Mto Ntwike kwani barabara ya Meli-Walla hadi Ntwike inayojengwa hata utakapokuwa imekamilika haitakuwa na maana kama daraja halitajengwa.
Awali Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba, Evance Kibona, akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi alisema wilaya hiyo imetengewa Sh.bilioni 6.836 ambazo chanzo chake ni kutoka katika Mfuko wa Barabara, ushuru wa mafuta na katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Kibona alisema hadi kufikia Januari 2024 Sh.bilioni 1.922 zimepokelewa ikiwa ni sawa na asilimia 28 ya Sh.bilioni 6.836 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.
"Kazi zinazoendelea kutekelezwa kupitia bajeti ya 2023/2024 ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.52 ,uwekaji wa taa za barabarani 55,ujenzi wa vipande vya barabara za zege kilometa 1.15,mitaro ya maji ya mvua na ujenzi wa makalavati katika barabara mbalimbali," alisema.
Naye Kaimu Meneja TARURA Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Paschal Mafuru, alisema wilaya hiyo imetengewa Sh.bilioni 2.513 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja.
Alisema hadi kufikia Januari 30, 2024, Sh.milioni 727.803 zilikuwa zimepokelewa sawa na asilimia 29 ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kazi za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara ambapo hadi sasa utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea umefikia asilimia 80.
Aidha, Mameneja hao walisema changamoto kubwa katika wilaya hizo ni upitishaji wa mifugo barabarani ambao umekuwa ukisababisha uharibifu wa barabara hususani za udongo na changarawe.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba miradi hiyo inayotekelezwa TARURA itaendelea kusimamia wakandarasi waliopewa zabuni ili iweze kukamilika kwa wakati kukingana na mikataba inavyoelekeza.
Kibasa alisema TARURA imeamua kufungua barabara ya Meli-Walla hadi Ntwike ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70 ili kuwarahisishia wananchi wa kata ya Ntwike ambao walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 40 kufuata huduma za afya na nyinginezo kwenda Kiomboi ambako ni makao makuu ya wilaya.
"Barabara ya Meli-Walla hadi Ntwike itakapokamilika wananchi wa Kata ya Ntwike sasa watakuwa wanasafiri umbali wa kilometa 23 tu kufika Kiomboi badala ya kilometa 40 ambako walikuwa wakilazimika kupitia Misigiri ndipo waende Kiomboi," alisema.
MWISHO
0 Comments