Header Ads Widget

RC MNDEME AKUTANA NA WAFANYABIASHARA WA SUKARI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme leo Jumanne Februari 27,2024 amekutana na kuzungumza na  wafanyabiashara wa Sukari ili kubaini sababu inayochangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

Wafanyabiashara aliokutana nao Mkuu wa Mkoa ni pamoja na wenye viwanda vya Sukari,mawakala pamoja na wenye maduka ya jumla na rejareja,ambao wametaja sababu mbalimbali zinazosababisha upungufu wa sukari

Wafanyabiashara wenye maduka ya jumla na rejareja wametaja sababu mbalimbali zinazowafanya kupandisha bei ya sukari ikiwemo gharama kubwa wanayonunulia  kutoka viwandani.

Akizungumzia changamoto ya Sukari Meneja wa kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar kanda ya ziwa Bwana Hassan Burhan Abdulkarim amesema Mvua za El-nino zimesababisha uzalishaji kushuka kutokana na mitambo kushindwa kuingia kwenye mashamba  baada ya kujaa maji.

“Suala la changamoto ya Sukari ni tatizo la kiukanda misimu hii miwili mitatu nyuma Mvua zimenyesha nyingi sana kupita kiasi ambazo Mvua hizo zimepelekea Mashamba kujaa Maji na Mashamba yakishajaa Maji Mashine zile za kupakia na Trekta za kutoa Mua ndani ya Shamba kupeleka kiwandani kwa ajili ya kusaga haziwezi kuingia tena mashambani, lakini Sukari inahitajika ni kipi kifanyike tufunge kiwanda au tutafute mbadala mbinu mbadala ni kubeba Mua begani kampuni imefanya hizo jitihada imeshaajili zaidi ya watu elfu saba kwa ajili ya kubeba Mua ndani ya Shamba  mpaka kwenye kiwanda”.amesema Meneja Hassan

Wafanyabiashara hao wameishauri serikali kuhakikisha inakuwa na utaratibu wa kuweka akiba ya kutosha ya bidhaa hiyo kabla  ya uhaba kutokea ikiwa ni pamoja na ushirikishaji wadau kwenye upangaji wa bei ya sukari.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa bidha hiyo kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga itashughulikia changamoto ya upungufu wa Sukari inayosababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

“Tunamuangalia yule mwananchi wa chini mkulima wa chini je anaweza kumudu shilingi elfu nne shilingi elfu tano kwa kilo moja ya Sukari ebu fikiria kilo moja ya Sukari kwa familia ya kawaida ni watu 8, Sukari ni muhimu sana kwetu Sukari siyo anasa Sukari siyo sterehe Sukari ni bidhaa muhimu na hasa katika kipindi hiki cha Kwarezima na tunapoenda kwenye mwezi mtukufu lakini pia kwa matumizi yetu ya kawaida ya nyumbani niseme tu kwamba maoni na ushauri wetu nimeupokea ninaomba mniachie niufanyie kazi”.amesema RC Mndeme

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita.

Aidha siku chache zilizopita Matukio Daima ilizungumza na baadhi ya wafanya Biashara wakiwemo mama lishe Mkoani Shinyanga,ambao waliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto ya upungufu wa Sukari ambayo imechangia kuwepo kwa mfumko wa bei.

Walieleza kuwa  hivi karibuni bei ya Sukari imepanda kutoka elfu 2800 hadi elfu nne (4000) kwa kilo moja na kwamba upatikanaji wake ni mgumu.

Wafanyabiashara walisema  hatua hiyo imechangia kupungua kwa wateja na kuathiri mapato katika Biashara zao za kila siku huku wakiiomba serikali kushughulikia changamoto hiyo haraka ili kuondoa usumbufu unaojitokeza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza kwenye kikao chake na wafanyabiashara wa Sukari Mkoani Shinyanga Februari 27,2024. 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza kwenye kikao chake na wafanyabiashara wa Sukari Mkoani Shinyanga Februari 27,2024. 




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI