Header Ads Widget

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI MANISPAA YA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme leo Februari 28,2024 ameanza ziara yake ambapo amesikiliza, kutatua kero na changamoto mbalimbali zaidi ya 50 za wananchi wakazi wa  Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Changamoto hizo zinagusa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Maji, Elimu, Ardhi pamoja na miundombinu ya Barabara.

Wananchi hao pamoja na mambo mengine wamehoji ni lini serikali itakamilisha ujenzi wa soko kuu la Mkoa wa Shinyanga ambalo lilitarajiwa kukamilika Mwaka jana mpaka sasa halijakamilika, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ametumia nafasi hiyo kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha soko hilo linakamilika kufikia Tarehe 30,05 Mwaka huu 2024.

Pamoja na changamoto mbalimbali zilizowasilishwa leo, wananchi wameendelea kuitaka serikali kuboresha miundombinu ya Barabara kutoka Ndala kuelekea Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambapo wamesema ni muhimu Barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa usumbufu unaojitokeza na kusababisha ajali mbalimbali.

Katika mkutano huo wa hadhara kero na changamoto nyingi zimetokana na migogoro mbalimbali ya ardhi na kwamba mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme katika ziara hiyo ameongozana na wataalam mbalimbali wakiwemo wakuu wa idara ambapo  changamoto za wananchi zimetolewa ufafanuzi.

Pia wananchi wameikumbusha serikali kuharakisha zoezi la mikopo inayotolewa na Halmashauri kwani wengi wao wamekuwa wakijiingiza kwenye mikopo yenye riba kubwa (Mikopo umiza au kausha damu) na kupelekea kukimbia familia zao ambapo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amewaomba wananchi kuwa wavumilifu na kwamba serikali bado inaboresha mfumo katika mikopo ya Halmashauri.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema zoezi la kupokea kero za wananchi linaendelea ambapo katika ziara yake kesho Alhamis Februari 29 kuanzia majira ya saa tano asubuhi atakuwa katika Manispaa ya Kahama.

RC  Mndeme pia  Machi mosi, 2024  atazungumza na wananchi wa Halmashauri ya Msalala kupitia Mkutano wa hadhara  ambapo saa tano asubuhi atafanya Mkutano wa hadhara katika kata ya Kakola, na baadaye Saa nane mchana atazungumza na wananchi wa kata ya Segese.

 

Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga akiwasilisha kero yake kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi leo Jumatano Februari 28,2024.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI