Mwandishi wetu- DAR
VIONGOZI wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) wamesema kuna upungufu mkubwa katika utengenezaji wa sera za serikali kwa jamii ya watu wenye ulemavu wa kusikia.
Kutokana na upungufu huo, jamii ya watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata wakati mgumu katika shughuli zao za kila siku ikiwa ni pamoja na kutokuwa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji yao.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mfumo wa uchangiaji wa ujenzi wa Kituo cha raslimali na mafunzo cha chama hicho mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini CHAVITA, Joseph Hizza alisema Kituo hicho kitakachojengwa Dodoma kitasaidia kuondoa vikwazo vilivyopo hata kwa watu wengine kutomtambua kiziwi.
Kituo hicho kikubwa Afrika Mashariki kinatarajiwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 6.4 sawa na Shilingi 17.5 bilioni za Tanzania.
Naye Mweyekiti wa CHAVITA, Selina Mayemba alisema kituo hicho pamoja na mambo mengine kitaboresha maisha ya jamii ya Viziwi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ambayo yataboresha maisha yao.
"Kupitia uzinduzi huu wa uchangiaji wa ujenzi niiombe jamii kupitia taasisi za serikali, watu binafsi, na taasisi za kimataifa ili kuchangia ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa viziwi na Taifa kwa ujumla.
"Mfumo huo wa uchangiaji ni rahisi na mwepesi kwa kila mmoja kuanzia kiwango cha Shilingi 100 hivyo kuwezesha watu wenye vipato mbalimbali kuchangia" alisema Selina.
Akiwasilisha andiko la mfumo huo wa uchangiaji unavyofanyakazi, Aneth Didas kutoka Kampuni ya Kolorio Innovation ya Dar es Salaam ambao ni waandaaji wa mifumo mbalimbali ya kidigitali, amesema kwa njia ya 'simu janja' pamoja na simu za kawaida, wachangiaji watakamilisha uchangiaji wa kiasi chochote cha fedha kwa kupitia simu zao za mkononi.
"Mchangiaji ataingia kwenye website ya Chavita ambayo ni www.deafdevelopment .or.tz atafuata maelekezo na kukamilisha changizo kupitia mitandao yote ya simu ambayo ni tgopesa, m-pesa, hallopesa, airtel money, Tpesa na Ezypesa ambayo ndiyo watanzania wote wanatumia." Alisema Aneth.
0 Comments