ZAIDI ya miezi mitatu hospitali ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wamekosa maji safi na salama na kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji katika hospitali jambo limesababisha zaidi ya wagonjwa wasita kushindwa kupona kwa wakati kutokana na ukosefu wa huduma hiyo kutoka MANAWASA
Akiongea kwenye kikao maalum cha kutathimini hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Nachingwea, kaimu Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Nachingwea Dr Ramadhan Maige alisema kuwa kukosekana kwa maji zaidi ya miezi mitatu kuleta madhara makubwa wagonjwa.
Dr Ramadhan alisema kuwa wamewafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya sita ambo hadi sasa vidonda vyao vinashindwa kupona kutokana na kutumia maji ambayo sio safi na salama wakati wa upasuaji.
Alisema kuwa iliwalazimu kufanya utafiti ili kugundua tatizo nini Kwa hao wagonjwa wakagundua kuwa maji ambayo wamekuwa wanayatumia wakati wa upasuaji yalikuwa na virusi (Bacteria) ambao wameleta madhara makubwa kwa wagonjwa hao
Hivyo aliwaomba MANAWASA kufungilia maji kwenye njia inayopeleka hospitalini ili kutokoa maisha ya binadamu wenzao ambao wanateseka kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Nachingwea ambaye ndio alikuwa mwenyekiti wa kikao Cha tathimini ya upatikanaji wa maji katika mji wa Nachingwea,Haji Mubaruk Balozi alikiri kukosekana kwa maji katika hospitali ya wilaya kunatokana na uzembe unaofanywa na MANAWASA.
DAS Balozi alisema kuwa haiwezekani wananchi wakawa wanateseka suala la maji na viongozi walioteuliwa na Rais Dr Samia wanaangalia mamlaka Moja tu ndio inaharibu taswira ya viongozi wa wilaya yote.
Alisema kuwa baada ya kuwaandikia barua MANAWASA ya kuwaita kwenye kikao na wadau,wananchi pamoja na viongozi mbalimbali maji yalianza kutoka siku hiyo hiyo jambo ambalo linaonekana mamlaka hiyo inafanya kazi Kwa mazoea.
DAS Balozi alisema kuwa wananchi wamekosa maji zaidi ya siku 90 halafu barua ya siku Moja inafanya maji yapatikane mji wote, haiwezekani ikiwa sahihi kuwakingia kifua MANAWASA wanafanya kazi kwa mazoea.
Naye kaimu Mkurugenzi wa MANAWASA Obadia Mtuya alisema kuwa tatizo lilikuwa umeme na sasa wameanza kutoa huduma hiyo kwa baadhi ya maeneo.
Mtuya alisema kuwa MANAWASA wanamaji ya kutosha hivyo umeme ukitengemaa kama ulivyo hivi sasa wananchi watapata maji Kila siku bila kuwa na Mgao.
Hata hivyo Bado viongozi wa wilaya ya Nachingwea na wananchi kwa pamoja hawajaridhishwa na majibu ya kaimu Mkurugenzi wa MANAWASA na wamemtaka kutafuta ufumbuzi zaidi wa kutatua kero ya maji kwa wananchi
0 Comments