NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Wananchi wa jiji la Arusha kata ya Muriet mtaa wa Mashariki wameangua kilio mbele ya katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Arusha Timoth Sanga kutokana na kukosekana kwa huduma za kijamii ikiwemo Maji, Umeme, Shule na barabara.
Hali hiyo imejitokeza baada ya katibu huyu kutembelea Mtaa huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea kata zote 20 na mitaa 154 ya jiji hilo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majibu.
Elizabeth Delton alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa na kero ya shule ambapo watoto wao wanatembea umbali wa takriban kilometa 6 kwenda shule ya msingi Terrat kwa kipindi cha kiangazi huku masika wakibaki majumbani kutokana na mafuruko yanayopita katika korongo lililopo mtaa huo ambayo ndio njia yao kuu ya kuweza kufika shuleni.
“Tunaiomba serikali kama kuna uwezekano mtusaidie shule, watoto wetu wanaenda mbali mtoto akitoka asubuhi saa 12 anafika saa 2, anakuta wanafunzi wenzake wameshaingia darasani, muda wa kurudi mtoto anayetoka saa tano anafika hapa saa nane,” Alisema mwananchi huyo.
Alifafanua kuwa pamoja na shule kuwa mbali, mvua ikinyesha maeneo ya mijini kinachoenda kwa ni mafuriko ambapo watoto wanashindwa kuvuka hivyo kupelekea watoto kuwa upande mmoja wa korongo na wazazi upande mwingine wakiwasihi watoto wao wasivuke ili wasibebwe na maji na wakati mwingine maji yakiwa mengi wanakaa hadi usiku mpaka yatakapopungua ndipo wawavushe.
Aliendelea kusema kuwa pia wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo wamekuwa wakifuata maji umbali mrefu wa saa tatu kwenda na kurudi na wakati mwingine wanakosa ambapo maji wanayoyatumia ni maji yayapita katika korongo yanayotoka viwandani ambayo sio safi na salama kwa matumizi ya majumbani.
“Kama kweli sisi ni wananchi kama wananchi wengine katika maeneo mengine maana tunaonekana kama tupo porini mtuletee angalau bomba kubwa, kwasasa kinachotusaidia ni maji ya mvua lakini bado tunalia na nyie tuleteeni angalau yale mabomba mtu anaweza kuvuta nyumbani kwake ili hata yakija usiku mtu unaweza kufungu kwasababu upo hapo hapo,”Alisema Elizabeth.
“Baba tunaomba utusaidie, peleka hiki kilio chetu, hii kero ya maji, shule watoto wanakufa wanapepwa na maji kila siku tunazika baba tunaomba utusaidie, fikisha kilio chetu hiki kwa Rais Mama Samia, tunaomba msaada wenu, tunaishi porini huku hatuna namna, hatuna jinsi,” Aliongea huku akilia Mwanachi huyo.
Gabriel Kalmae alieleza kuwa kero nyingine waliyonayo ni barabara ambapo kinachoshangaza zaidi mlima wenye kokoto wanao lakini malori kotoka maeneo mengeine yanaenda kuchukua katika mtaa wao na kupeleka kwebye barabara zao lakini kwao hatutengenezwi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini Timoth Sanga (Katikati) akikagua barabara, amembatana na baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya kata ya Muriet
"Miundombinu ya barabara ni mibovu kupindukia, mvua hapa ikinyesha hata kutembea kwa miguu ni kazi, piki piki hazipiti wala magari lakini pia maji yakishajaa kwenye korongo hakuna kupita, ni maumivu makali miundombinu ya barabara imekaa vibaya na nafikiri mmeona wakati mnakuja na mvua ingenyesha msingefika,” Alisema.
“Kuna barabara kuwa ya kutoka Nadosoito kupitia kwa Nginaai ile ni kama zizi la Ngombe haipitiki kabisa na haijawahi kuwekwa moram ata siku moja, ina mashimo na inalaza maji watoto wadogo wa darasa la kwanza na la pili hawawezi kupita mpaka waendw na wazazi wao, mzazizi naye ni kama anaenda kusoma atoke asubuhi mpaka saa nne ndipo arudi, mchana tena amfuate mwanafunzi kisa barabara kwahiyo tunaomba serikali iliyopo madarakani itusaidie, Rais wetu Samia atusikie,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa elimu kata ya Muriet Mwalimu Noel Mbaruku kuhusiana na suala la shule aliwajubu wananchi kuwa changamoto hiyo ipo na wamekuwa wakiliongelea suala hilo kwenye vikao ili eneo hilo liweze kupata shule na limeshafika kwa mkurugenzi wanachosubiri ni kupata mwelekeo.
Diwani wa kata hiyo Fransis Mbise Alisema kuwa wamepeleka kero za wananchi na zinafanyiwa kazi ambapo katika suala la maji wamepelekewa mabomba ya muda (temporary) katika vituo vitatu ambapo na wameahidiwa maji yatafunguliwa na wabanchi hao wataanza kupata maji safi na salama.
Mhandisi wa Maji kanda ya Muriet Haksad Makyao kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Arusha (AWUSA) alisema kuwa kulikuwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu ambapo wameangalia uwezekano wa kuweza kuokoa kwa kipindi cha muda mfupi wakapendekeza Domestic poin(virula) tatu ambapo kwasasa bado wanatoa upepo kwenye mabomba na baada ya hapo wananchi hao watapata maji safi na salama.
Naye Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Arusha mjini Timoth Sanga alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majibu ambapo aliwataka wananchi kutokaa kimya bali wapaze sauti kwani mambo hayo yanawezekana.
“Mkikaa kimya msiposena ndo basi kwani kuna watu wengine huku kwenye uongozi wana yao kwanza kabla ya wananchi, na mnapochagua vionguzi muwe mnapima sio anakuja tuu mtu anakupa elfu tano, elfu kumi na wewe unamchagua huyo atashindwa kukutetea kwasababu akishapata atarudisha kwanza hela yake ndipo ashughulike na yenu baadae.
Aidha aliwataka kuhusiana na suala la shule wawape muda angalau hadi mwezi wa tatu kwani wataalamu wameshafika katika eneo hilo na wamesema fedha ipo hivyo ni suala la kufuatilia tuu ambapo baada ya kupatikana eneo na shule kujengwa wanafunzi wanaonde umbali mrefu watahamishiwa katika shule hiyo.










0 Comments